Na Lydia Lugakila, Muleba
Wahitimu wa chuo cha Muleba Lutheran Vocational Training Centre (MLVTC) 2024 kutoka Wilayani Muleba Mkoani Kagera wametaja kufanikiwa katika kupata ujuzi kwa fani walizofundishwa chuoni hapo ikiwa ni pamoja na nidhamu.
Wahitimu hao wamebainisha hayo kupitia lisala yao kwa mgeni rasmi katika mahafali ya 12 ya chuo hicho yaliyofanyika Wilayani humo.
Katika lisala iliyosomwa na mmoja wa wahitimu hao aitwaye Auson Didace mbele ya mgeni rasmi ilieleza mafanikio waliyoyavuna chuoni hapo kuwa ni pamoja na chuo hicho kuzalisha wataalam wazuri katika taaluma ya Teknolojia ya Habari na mawasiliano(TEHAMA) na fani ya umeme, uboreshaji katika sekta ya kilimo hasa cha mboga mboga na matunda mradi wa ufugaji wa kuku ambapo Vijana wengi waliopita chuoni hapo wamefanikiwa kupitia fani hizo.

Kupitia lisala hiyo Vijana hao walisema kuwa wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo kukosa baadhi ya vitendea kazi kwa ajili ya masomo yao, ufinyu wa darasa la umeme vifaa vya mpira, kukatikatika kwa umeme jambo linalokwamisha kujisomea.
Aidha katika mapendekezo yao wahitimu hao wameiomba Serikali kutoa mkopo kwao ili wanapohitimu waweze kujiajiri wenyewe ambapo wametaka hoja hiyo ijadiliwe katika majukwaa mbali mbali huku wakieleza kuwa elimu waliyoipata chuoni hapo itakuwa msingi wa maisha yao na jamii kwa ujumla wakiongozwa na nidhamu na uzalendo kwa ajili ya Nchi yao.
Akijibu lisala hiyo Afisa Masoko wa Dayosisi ya Kaskazini Magharibi Danson Kateme ambaye amekuwa mgeni rasmi niaba ya karibu Mkuu wa Dayosisi hiyo aliwasihi wahitimu hao kuwa wabunifu kwa kutengeneza ajira kwa kuangalia fursa zilizowazunguka ikiwemo kujipanga kuendana na kasi ya dunia ya Sayansi na Teknolojia, kutokukumbatia fani pia wajiendeleze.
Kateme alichukua fursa hiyo kuwapongeza wazazi wa wahitimu hao waliojinyima ili watoto wao wapate elimu ambapo pia alimpongeza Mkuu wa chuo hicho wa sasa na Mkuu wa chuo aliyestaafu kwa kazi ya kuwanoa Vijana hao kinidhamu huku akiwasihi Vijana hao kujiepusha na magenge yasiyofaa yatakayowafanya kutosonga mbele.
Hata hivyo naye Mkuu wa chuo hicho Benetson Kamugisha aliwapongeza na kuwashukuru walimu waliowaandaa vizuri Vijana hao kitaaluma na nidhamu huku aliwasihi wazazi kuendeleza nidhamu hiyo.
“Naamini kupitia mafunzo katika fani kuu mbili za TEHAMA na Umeme Vijana wetu wameiva pia wapo vizuri ki nidhamu”alisema Mkuu wa chuo hicho.
Hata hivyo Kamugisha aliwahimiza wahitimu kukumbuka kujiongezea thamani kwa kujiendeleza, kujielimisha na kuwa wabunifu wakati wote katika fani zao kuendana na kasi ya dunia ya Sayansi na Teknolojia.
