Uokozi unaendelea leo ghorofa lililoporomoka Kariakoo jana, waliokufa…

SHUGHULI za Uokoaji wa watu waliofukiwa na kifusi baada ya jengo la ghorofa kuporomoka Kariakoo jijini Dar es Saalaam, limeendelea leo Jumapili ya Novemba 17, ingawa Mamlaka zimetofautiana juu ya idadi ya waliofariki kati ya wanne na watano, huku idadi ya waliookolewa wakiwa hai wakitajwa kuwa 70.

Jana usiku, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Albert Chalamila, alisema waliofariki ni wanne, huku Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Peter Mtui, mapema jana jioni alisema waliofariki ni watu watano.

Kwa mujibu wa Chalamila, kufikia jana jioni watu waliofariki walikuwa ni wanne, huku akibainisha kuwa kati yao hakuna aliyefariki kwa kukosa hewa, bali vifo vyao vilitokana na aidha kuangukiwa na kuta za jengo, kuchomwa na nondo, kuangukiwa na tofali au kujipigiza.

Chalamila alifafanua kuwa, kati ya watu 70 waliookolewa, 40 walipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambako 35 kati yao walitibiwa na kuruhusiwa, huku wengine 30 wakipelekwa Hopsitali za Amana na Mnazi Mmoja, ambao kati yao 28 walitibiwa na kuruhusiwa, huku wawili wakilazwa.

Aidha, taarifa za RC Chalamila zimethibitisha kuwa uokozi unaendelea leo Jumapili na wamefanikiwa kumuokoa mtu mmoja akiwa hai, na kwamba mawasiliano na watu waliofukiwa yaliendelea hadi jana usiku, wakiomba msaada ambapo jitihada za kuwafikishia Oxygen na Glucose zilikuwa zikifanywa.

“Kwa wale wachache ambao wamepata majanga ya kifo, inavyoonekana mpaka sasa walifariki dunia kwenye tukio lenyewe kwa maana wakati wa kudondoka kwa kudondokewa na jiwe ama amechomwa na nondo, lakini mpaka muda huu waliokufa kwa kukosa hewa bado hatujaipata taarifa hiyo,” amesema leo Jumapili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *