NMB yatoa fidia ya Bil. 1.117 kwa wakulima wa tumbaku Tabora

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe (wa pili kushoto) akipokea mfano wa hundi yenye thamani ya zaidi ya Sh.Bilioni 1.117 kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wa pili kulia), Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Bima ya UAP, Nelson Rwihula (wa tatu kushoto) ikiwa ni fidia kwa wakulima 2,226 wa tumbaku katika hafla iliyofanyika Jijini Dar es Salaam leo Novemba 13, 2024. Kulia ni Kamishna wa Mamlaka ya Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware na kushoto ni Afisa Mkuu Wateja Binafsi na Biashara NMB, Filbert Mponzi. (Na Mpiga Picha Wetu).

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe, ameipongeza Benki ya NMB kwa kukabidhi fidia ya Sh. Bilioni 1.117 kwa wakulima wa Tumbaku 2,226 kutoka Vyama vya Msingi (AMCOS) 22 mkoani Tabora waliokopa kwenye taasisi hiyo, iliyotenga zaidi ya Sh. Bilioni 291 za Mikopo ya Kilimo cha zao hilo kwa msimu wa 2024/2025.

Waziri Bashe ametoa pongezi hizo wakati akipokea hundi ya mfano kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna, naye kuikabidhi kwa Mwakilishi wa Wakulima na Mwenyekiti wa AMCOS ya USAGUZI, Ally Mrisho, mbele ya Dk. Baghayo Saqware, ambaye ni Kamishna wa Mamlaka ya Bima Tanzania (TIRA).

Akizungumza wakati wa hafla hiyio, Waziri Bashe alisema NMB na Kampuni ya Bima ya UAP wameonesha mfano wa kuigwa kwa kukubali kuchukua hatari na kutoa Bima za Kilimo, sekta aliyoitaja kuwa ngumu zaidi kukopesheka kutokana na uwingi wa viatarishi vinavyoizunguka sekta na wadau wake, hasa wakulima.

“Kuthibitisha dhamira ya dhati ya NMB katika kukuza sekta ya kilimo, ilitoa mikopo yenye thamani ya dola milioni 60, takribani Sh. Bilioni 150 hivi. Jumla ya AMCOS 256 zilinufaika na mikopo hiyo, lakini athari zikawafikia wakulima kutoka AMCOS 22, wanaolipwa fidia hii kutoka NMB na UAP.

“NMB wamekuwa vinara wa utoaji wa fidia za bima za kilimo na kila mmoja hapa anafahamu kwamba hakuna sekta ngumu kukopesheka kama kilimo, kutokana na viatarishi vya sekta hiyo, lakini NMB na UAP wamesimama imara kuhakikisha wakulima wanaelewa umuhimu wa bima hizi.

“Serikali tumejipanga katika kufanikisha ‘Comprehensive Agricultural Scheme,’ bila hiyo hakuna mkulima anayeweza kukopesheka, TIRA iharakishe mchakato huo, kwani kila zao lina tabia zake na vihatarishi vyake na Serikali inajipanga kuhakikisha tunajenga mfumo wa bima kwa kila zao kulingana na vihatarishi vyake,” alisema.

Bashe alibainisha ya kwamba tumbaku limekuwa zao muhimu kwa uchumi wa taifa na kuwa miaka mitatu nyuma Tanzania haikuwa mzalishaji mkubwa, lakini kutokana na mchango wa taasisi za fedha zikiongozwa na NMB, sasa Tanzania ni ya pili kwa uzalishaji wa tumbaku Arika.

Akaongeza ya kwamba, licha ya athari zilizolipiwa fidia  hiyo ya Bil. 1.117, mapato ya jumla ya zao la tumbaku kwa msimu wa 2023/24 ulikuwa ni Sh. Bil. 724 kutoka Sh. Bil. 717 za msimu wa 2022/2023 na kwamba msimu huu wa 2024/2025, matarajio ya pato la jumla kwa wakulima litakuwa Sh. Trilioni 1.7 

Akizungumza katika hafla hiyo, Bi. Zaipuna alisema licha ya kukabidhi hundi yenye thamani ya Sh. Bilioni 1.117 ikiwa ni fidia kwa wakulima wa tumbaku na Vyama vya Ushirika na Masoko (AMCOS) mkoani Tabora waliokopa katika benki hiyo, NMB imetenga kiasi cha Sh. Bilioni 291.6 kwa ajili Mikopo ya Kilimo hicho msimu huu.

Alisema wakulima hao walikatia bima mikopo yao kwa Kampuni ya UAP, na hiyo ni mara ya pili kwa NMB na UAP kutoa fidia ya bima kwa wakulima wa Tumbaku wa mkoa wa Tabora, ambapo mwaka jana walikabidhi fidia ya Sh. Mil. 374 kwa wakulima 400 kwa sababu hizo hizo za hali ya hewa kuathiri kilimo chao.

“Wakulima tunaowafidia leo ni mmoja mmoja na ambao kupitia AMCOS zao, walichukua mikopo ya kilimo cha Tumbaku NMB, ambayo ilikuwa na Bima kutoka Kampuni ya UAP na hili linakuja baada ya kukamilisha upembuzi na tathmini thabiti na washirika wetu hao,” alisema Bi. Zaipuna na kuongeza:

“Wakulima hawa walikumbana na athari za kuharibiwa mashamba na mazao yao katika kipindi cha mvua kubwa pamoja na mvua za mawe, baada ya tathmini kufanywa na wataalamu, ripoti ilitoka na sasa Kampuni ya Bima ya UAP kupitia NMB, tupo tayari kukukabidhi hundi ya fidia hiyo kwa niaba ya waathirika.” 

Bi. Zaipuna aliishukuru UAP insurance kwa kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa wakati na wakulima wanapata stahiki zao na kwamba NMB ndio kimbilio sahihi litakalowasaidia waathirika katika kufuatilia fidia zao za Bima na kuzipata ndani ya muda muafaka, kuwawezesha kuendelea na shughuli zao.

Afisa Mtendaji Mkuu huyo aliwapongeza wanufaika hao kwa kukata bima na NMB, benki aliyosema imetenga kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 108 (sawa na Sh. Bilioni 291.6) kwa ajili ya mikopo kwa wakulima wa tumbaku tu katika msimu huu wa mwaka 2024/2025 na kuwakaribisha wakulima kuchangamkia fursa hiyo.

“NMB ni sehemu sahihi ya kuchukua mikopo ya kilimo – mnyororo unaojumuisha kilimo chenyewe, uvuvi na ufugaji, kwani tuna riba nafuu ya asilimia 9 tu kwa mwaka na uhakika wa fidia yanapotokea maafa kama haya. Tunaishukuru Wizara ya Kilimo kwa kuendelea kushirikiana vyema na NMB katika Sekta ya Kilimo,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *