SIKU ya kufa nyani, miti huteleza, hii ni semi ya Kiswahili iliyotumiwa na Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, akielezea kipigo alichopata yeye na kikosi chake kutoka kwa Tabora United, kuwa kimetokana na kukosekana kwa mabeki wote wanne wa kikosi cha kwanza, Yao Kouassi, Shadrack Boka, Dickson Job na Ibrahim Hamadi ‘Bacca.’

Yanga, wakiwa na rekodi ya kufungwa bao moja na kupoteza mchezo mmoja kati ya 9 ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, walishuka Dimbani kuwaalika Tabora United, bila nyota wao hao, na dakika zao 90 Dimbani Azam Complex zikaishia kwa kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Warina Asali wa Tabora.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Gamondi raia wa Argentina, amesema siri ya kupoteza pambano hilo ni kukosekana kwa nyota wake wanne wa ulinzi, huku sababu nyingine ikiwa ni upotevu wa nafasi walizotengeneza, ikiwamo kukosa penalti ya dakika ya 44 iliyopigwa na Stephanie Aziz Ki.
“Tumekubali matokeo na Tabora United wamestahili, tulikuwa na kikosi kilichocheza bila mabeki wake wanne wa kikosi cha kwanza kutokana na majeruhi na kutumikia adhabu, na unapokosa wachezaji wako muhimu, unahitaji kuwa makini na kutumia kila nafasi unayozalisha mchezoni, vitu ambavyo hatukuvifanya.
” Tulitengeneza nafasi, tulitawala mchezo, lakini umakini katika eneo la mwisho imetugharimu, hasa ukizingatia tukicheza bila nyota wetu muhimu, ikiwemo pia kuumia kwa Aziz Andabwile. Tunarudi mazoezini kuyafabyia kazi makosa yaliyotughatimu ikiwemo kutazamia hali za majeruhi wetu. Tutarudi tukiwa bora zaidi na kuendelea na mbio za ubingwa,” alisema Gamondi.
Mabao ya Tabora United katika mechi hiyo yalifungwa na winga Francis Chiloka mabao mawili katika dakika za 20 na 45, Hulu bao la tatu likiwekwa kambani na Nelson Munganga dakika ya 77.

Bao la kuvutia machozi la Yanga limefingwa na Clement Mzize dakika ya 90 ya mechi hiyo, iliyoisha kwa Chikola kutangazwa Mchezaji Bora Bora wa Mechi (MoTM).
Yanga iliwavaa Tabora United ikiwakosa mabeki wake wanne wa kikosi cha kwanza, Dickson Job (kadi tatu za njano), Yao Kouassi (majeruhi), Ibrahim Hamadi ‘Bacca’ (kadi nyekundu) na Shadrack Boka (majeruhi), huku Aziz Andabwile aliyepangwa ulinzi wa kati akiumia mapema dakika ya 10 na kushindwa kuendelea, hivyo nafasi yake kuchukiliwa na Salum Aboubakar ‘Sure Boy.’