NMB yadhamini Mkutano wa TAMSTOA kuzindua Kanzidata ya Dereva Tanzania

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori (TAMSTOA), Chuki Shabani, akitoa hotuba yake wakati wa mkutano wa utambulisho wa Kanzidata ya Dereva Tanzania uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo.

Mkuu wa Idara ya Biashara wa Benki ya NMB, Alex Mgeni, akizugumza kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo wakati wa utambulisho wa Kanzidata ya Dereva Tanzania ya Chama cha Wamiliki wa Malori (TAMSTOA).


NA MWANDISHI WETU

BENKI ya NMB imedhamini Mkutano Chama cha Wamiliki wa Malori Wadogo na wa Kati (TAMSTOA), uliotumika kuitambulisha na kuizindua Kanzidata ya chama hicho iitwayo Dereva Tanzania, huku ikiwahakikishia Vyama vya Sekta ya Usafirishaji uwepo wa huduma za kimkakati zinazolenga ustawi wao kibiashara.

Dereva Tanzania ni mfumo wa kisasa uliobeba suluhu ya changamoto zote zinazowakabili wamiliki na madereva nchini, ukilenga kuboresha na kuleta tija na ufanisi katika Sekta ya Usafirishaji nchini, ubunifu uliotokana na ushirikiano wa karibu baina ya Vyama vya Maederva na TAMSTOA yenyewe.

Akizungumza wakati wa uzinduzi na utambulisho wa Dereva Tanzania, Mkuu wa Idara ya Biashara ya NMB, Alex Mgeni, aliipongeza TAMSTOA kwa mapinduzi chanya ya kimfumo yaliyozaa Kanzaidata hiyo inayoenda kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili wamiliki na madereva wao.

Mgeni alikiri kuvutiwa sio tu na mfumo mpya uliopo kwenye Kanzidata hiyo, bali uwepo wa wanawake wamiliki wa malori na wanawake madereva, na kusema taasisi yake inajisikia faraja kuona kinamama nao wamekuwa wadau muhimu Sekta ya Usafirishaji, akilitaja kuwa ni kundi walilo na ajenda za kimkakati nalo.

“Tuna huduma nyingi zinazolenga kumnyanyua mwanamke kiuchumi, ambazo ni raifiki kwa kundi hilo, ambalo ni mhimili wa uchumi wa familia, jamii na taifa kwa ujumla wake,” alisema Mgeni katika hafla hiyo na kuongeza kuwa:

“Tukio hili ni kubwa, sifa za Kanzidata hii zinatupa matumaini makubwa kwamba miaka miwili ijayo, tutakuwa tunazungumza vitu tofauti ju ya Sekta ya Usafirishaji. Sisi NMB tutashirikiana kusaidia kuwawezesha wamiliki, madereva na wadau wote wanaoguswa na mfumo huu, ambao ni wadau wetu kibiashara.

“Awali tulikuwa tunakopesha vifaa kazi, ikiwemo malori kwa wamiliki kwa mikopo ya miaka mitatu, lakini sasa tumeongeza muda hadi miaka mitano na hii ni kutokana na tunayojifunza kwenu tunapokutana nanyi katika masuala yenu kama haya.

“NMB tunaendelea kufanya vizuri na kukuza mtaji wetu, Tanzania hakuna benki nchini inayoweza kuvuka uwezo wetu katika kumkopesha mteja mmoja mmoja, tunaweza kukopesha hadi Sh. Bilioni 400 kwa mteja mmoja, mtu anapohitaji zaidi tunalazimika kujenga ushirikiano na benki nyingine, ingawa nazo zina mitaji midogo.

Alienda mbali zaidi kwa kusema madereva wengi nchini hawana bima, na kwamba NMB inazo kampuni washirika za bima nyingi, ili kuwawezesha wateja wao kupata bima za nafuu na rahisi kulingana na mahitaji, huku akiipongeza TAMSTOA kwa uzinduzi huo muhimu kwa ustawi wa wamiliki na madereva wa malori Tanzania.

Awali, Mwenyekiti wa TAMSTOA, Chuki Shabani, alisema lengo kuu la Kanzidata hiyo ni kuunda mfumo wa kisasa utakaohifadhi taarifa zote za madereva kuanzia mafunzo yao, uzoefu wao na rekodi nyinginezo za ajira na utendaji kazi wa wamiliki ili kurahisisha mchakato wa kusaka ajira na kusaka waajiriwa.

“Mfumo huu utasaidia mambo yafuatayo; Moja kuongeza uwazi wa uwajibikaji kwa kuwa na rekodi za kina za madereva, kujua madereva stadi, wenye mafunzo na waadilifu.

“Mbili ni kuboresha mafunzo na maendeleo ya madereva, ambapo taarifa zilizopo zitatumika kuonesha maeneo yanayohitaji mafunzo zaidi ya kuboresha ujuzi wa madereva, na tatu kuimairisha usalama barabarani, tukiamini kuwa na madereva waliohitimu vizuri, wenye rekodi safi, kutapunguza ajali na kuongeza usalama wa abiria na mizigo.

“Nne, kurahisisha mchakato wa uajiri na uthibitisho wa madereva, ambapo waajiri watakuwa na mawanda mapana ya kuthibitisha sifa na uzeoefu wa madereva kabla ya kuwapa ajira na kupunguza mashaka ya kuajiri wasio na sifa,” alieleza Shabani.

Alitaja faida ya tano ya Kanzidata hiyo kuwa ni kurahisisha ajira kwa dereva, ambapo kutakuwa na dirisha maalum litakaloorodhesha madereva waliohitimu mafunzo na kuthibitishwa kuwa na sifa na uzoefu wa kuajiriwa, faida ya sita ikiwa ni kuhakikisha kila dereva mwnye sifa anapata ajira.

“Pia, mfumo utawezesha kulinda haki za madereva na kumlinda dereva kisheria na itaonesha kila mmiliki anawajibika kutoa mkataba wenye sifa kwa madreva,” alisisitiza Shabani na kubainisha kwamba Dereva Tanzania ni fursa inayohitaji ushirikiano, hivyo kutoa wito kwa wadau kushirikiana katika kufanikisha utendaji kazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *