
Gaspar Chacha aliyetengeneza biodiesel.

Jasem Abdallah, Aarush Gada na Faraj Mohamed waliotengeneza gari.

Aisha Saidi Neema Charles na Sabrina Mohamed walitengeneza barabara kwa kutumia chupa za plastic.

Presley Meleczedec Patricia na Tracey waliobuni nishati itokanayo na mtikisiko wa hatua za binadamu.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa AMIS Dr Ishaan Ahmad Khan.

Kaimu Mkuu wa Shule ya Kimataifa wa Arusha Meru, Mustapha Omary Nassoro.
Na Mwandishi Wetu
Shule ya Kimataifa ya Arusha Meru (AMIS) ilifanya onyesho la elimu, ujuzi na ubunifu lililovutia wanafunzi kutoka shule mbalimbali za kimataifa.
Hafla hiyo iliyofanyika Novemba 1, 2024 kwenye shule hiyo iliyopo jijini Arusha ilijumuisha miradi ya kisayansi inayolenga kutatua changamoto za kijamii na mazingira, na kuonesha ubunifu wa wanafunzi.
Katika onyesho hilo, wanafunzi wa shule ya AMIS walionyesha miradi mbalimbali, ikiwemo utengenezaji wa biodiesel kutoka mafuta ya mboga.
Wanafunzi Gaspar Chacha, Shedrack Mbasha, na Shawn Antony walielezea jinsi walivyotumia potasiamu hydroxide na methanol kuunda nishati mbadala inayopunguza uzalishaji wa hewa chafu.
“Biodiesel ni njia nzuri ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Chacha.
Wanafunzi wengine walionesha ubunifu wao kwa kutumia piezoelectric, vifaa vinavyoweza kubadilisha mitikisiko kuwa nishati.
Presley Meleczedec, Patricia, na Tracey walifafanua jinsi wanavyoweza kukusanya nishati kutokana na mitikisiko ya watu katika maeneo ya umma.
“Hii itasaidia katika kuunda nishati mbadala na kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati vinavyotokana na mafuta,” walisema.
Miradi ya ajabu pia ilitolewa na wanafunzi wa shule ya St. Jude. Aisha Saidi, Neema Charles, na Sabrina Mohamed walitengeneza barabara kwa kutumia chupa za plastiki.
Walisema, “Tumejenga barabara hii ili kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuboresha miundombinu vijijini.” Hii ni hatua muhimu katika kutatua tatizo la taka za plastiki na kuboresha maisha ya watu.
Wanafunzi Jasem Abdallah, Aarush Gada, na Faraj Mohamed walikamilisha mradi wa gari dogo.
Jasem alisema, “Tumetumia chuma kutengeneza injini ya Honda ambayo inaweza kuendeshwa na mtu mwenye uzito wa chini ya kilo 70.”
Gari hilo lina uwezo wa kukimbia kilomita 140 kwa saa na linatumia lita tatu za mafuta kwa kila kilomita 180.
Ofisa Mtendaji Mkuu, (CEO) wa AMIS, Dr. Ishaan Ahmad Khan, alisisitiza umuhimu wa ubunifu katika elimu.
“Tunataka kuwapa wanafunzi fursa ya kuonyesha uwezo wao katika masuala ya kisayansi. Onyesho hili ni njia nzuri ya kuwapa motisha na kuwajengea uelewa mzuri wa sayansi,” alisema Khan.
Kaimu Mkuu wa shule, Mustapha Omary Nassor, aliongeza kuwa elimu ya sayansi ni muhimu kwa maendeleo ya jamii.
“Lazima tuweke juhudi katika kukuza uelewa wa sayansi ili wanafunzi wetu waweze kutatua matatizo yanayowakabili,” alisema Nassor.
Onyesho hili lilihusisha jumla ya miradi 300 kutoka shule mbalimbali ambapo wazazi na jamii walifika kuona kile watoto hao walichofanikiwa kutengeneza katika kuhamasisha elimu.
Wanafunzi walipata fursa ya kujifunza kutoka kwa wenzao na kupata mawazo mapya katika uwanja wa sayansi.
Hafla hiyo pia ilijumuisha zawadi kwa washindi wa miradi bora, ikiwa ni njia ya kuhamasisha ubunifu miongoni mwa wanafunzi. “Tunatarajia kuona matokeo chanya kutokana na miradi hii katika siku zijazo,” alisema Khan.
Kwa ujumla, onyesho la elimu, ujuzi na ubunifu limeonyesha juhudi za AMIS na shule nyingine katika kukuza elimu ya sayansi nchini Tanzania, na kuhamasisha vijana kufikiri kwa ubunifu ili kutatua changamoto za kisasa.