Golden Tulip, ASA Microfinance, wawasaidia wenye Saratani ya Matiti ORCI

NA MWANDISHI WETU

KATIKA kuhitimisha mwezi wa kujenga uelewa juu ya Saratani, Hoteli ya Golden Tulip Dar City Center, Taasisi ya ASA Microfinance Ltd na Hospitali ya Shifaa, wamekabidhi misaada mbalimbali ya vifaatiba kwa wanawake wenye Saratani ya Matiti wanaotibiwa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI).

Misaada hiyo imekabidhiwa Alhamisi Oktoba 31 kwa Taasisi ya Ocean Road, ambapo Golden Tulip, ASA na Shifaa, wamekabidhi vifaa tiba na pesa taslimu vyenye thamani ya Sh. Mil. 8 zilizochangishwa kupitia Matembezi Kutoa Elimu na Kujenga Uelewa wa Masuala ya Saratani ‘Walkathon,’ yaliyofanyika Oktoba 26.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo yaliyofanyika Ocean Road jijini Dar es Salaam, Meneja Masoko na Mauzo wa Hoteli ya Golden Tulip Dar City Center, Mariam Temba, alisema msaada wao ni mrejesho wa matembezi hayo yaliyolenga pia kuchangisha pesa za kununulia mahitaji ya kinamama hao.

“Tuko hapa kutoa mrejesho, wiki iliyopita tulifanya matembezi ya Kutoa Elimu na Kujenga Uelewa Juu ya Maradhi ya Saratani ‘Walkathon,’ ambayo tuliyatumia kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia ununuzi wa mahitaji ya taasisi hii na wagonjwa wake kwa ujumla.

“Tunashukuru matembezi yalifanyika na tukapata kiasi cha zaidi ya Sh. Mil. 8, ambazo tumezitumia kununua mahitaji ambayo tumeleta hapa leo kusaidia wodi za kansa na wagonjwa wetu, kupitia kiasi hicho tumenunua vifaatiba ambavyo tuliagizwa na taasisi na pesa iliyosalia inakabidhiwa kwa matumizi mengine,” alisema Mariam.

Kwa upande wake, Mkuu wa Rasilimali Watu na Utawala wa ASA Microfinace Ltd, Mohammed Omar Almasi, alisema taasisi yake ya kifedha inayojishughulisha na mikopo kwa wajasiliamali, ilichagua kushiriki Walkathon hiyo kwa sababu asilimia 99 ya wateja wao kina mama ambao ndio wahanga wa saratani ya matiti.

“ASA Microfinance tunatoa mikopo kwa wajasiriamali kote Tanzania Bara na Visiwani. Tuna wateja zaidi ya 300,000 na matawi 212, wengi wao ni wanawake na hili likatusukuma kushiriki matembezi hayo ili kutoa mchango wetu katika kusaidia matibabu ya mama zetu wanaotibiwa saratani hapa.

“Maradhi ya saratani ya matiti kwa wanawake yanahitaji uangalizi wa kina na ushirikiano na wadau kusaidia mahitaji yao na ndio maana ASA Microfinance, Golden Tulip Hotel na Shifaa Hospital, tuliandaa Walkthon ya kukusanya fedha za kusaidia kinamama wenye saratani ya matiti,” alifafanua.

Aidha, Taasisi ya Saratani Ocean Road, imeeleza kuwa aina hiyo ya Saratani inatibika endapo kama itawahiwa, hivyo imetoa rai kwa jamii kuwa na utamaduni wa kufanya uchunguzi wa awali wa Saratani ya Matiti ili inapobainika kuanza tiba haraka kama inavyotakiwa.

Hayo yameelezwa Bi. Mwamvita Saidi, ambae ni Mtumishi ORCI wakati wa hafla ya kupokea vifaa tiba kwa ajili ya Wagonjwa wa Saratani, vilivyotolewa na Hospitali ya Shifaa, Golden Tulip Dar City Centre pamoja na ASA Microfinance.

“Jamii inapaswa kuwa na utaratibu wa kukimbilia uchunguzi wa awali wa Saratani ili kuanza tiba haraka, niwatoe hofu Watanzania, wasiogope kwa sababu tiba ya Saratani haiwezi kupoteza maisha yao,” alisema Bi. Mwamvita wakati wa mapokezi ya vifaa tib ana pesa ziliztokana na matembezi hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *