Mfuko wa Taifa wa Maji waanika mafanikio, wananchi milioni 5.3 wanufaika

MFUKO wa Taifa wa Maji (NWF), umeeleza mafanikio iliyovuna katika kipindi cha uongozi wa Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan, ambapo imekamilisha utekelezaji wa miradi ya maji 354 kati ya Julai 2021 hadi Juni 2024, huku miradi ya maji 354 kati ya 998 iliyopokea fedha za mfuko huo, ikinufaisha wananchi milioni 5.3

Hayo yamo katika ripoti ya kurasa 34 ya NWF iliyotolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wake, Haji Mohammed, wakati mkutano na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, katika mfululizo wa Ofisi ya Msajili wa Hazina kukutanisha taasisi zilizo chini ya ofisi yake na vyombo vyua habari kueleza mafanikio yao.

Mfuko wa Taifa wa Maji umeanzishwa chini ya Sheria ya Usambazaji Majisafi na Usafi wa Mazingira Na. 05 ya Mwaka 2019, ikiwa ni Taasisi ya Fedha yenye Lengo la kutoa fedha za utekelezaji wa Miradi ya Usambazaji Majisafi kwenye maeneo yenye uhaba na Utunzaji wa Vyanzo vya Maji Nchini.

Uanzishwaji wa mfuko huo unalenga kuwa na uwepo wa chanzo cha fedha cha uhakika cha kutekeleza miradi mbalimbali ya maji, mfuko ambao umeanza kufanya kazi rasmi Mwaka 2015/2016 kwa mujibu wa sheria iliyotangulia kutajwa hapo juu.

Akizungumza wakati wa mkutano huo uliofanyika Oktoba 31 jijini Dar es Salaam, Haji Mohammed, alisema NWF katika Kuzindua Dirisha la Mikopo na kuanza kutoa Mikopo, hadi Julai 2024, jumla ya Sh. Bilioni 5.3 zimetolewa kama mikopo kwa Mamlaka za Maji.

“Takribani miradi 104 ya uhifadhi na uendelezaji wa Vyanzo vya Maji imetekelezwa ikijumuisha uhifadhi wa vyanzo vya maji zaidi ya 92 (zikiwemo chemichemi, vidakio vya maji, maziwa, mabwawa, mito na visima).

“Pia, ujenzi wa bwawa moja, ukarabati wa mabwawa saba, uchimbaji wa visima virefu zaidi ya 50, pamoja na kurudisha mito mitano iliyopoteza mikondo yake, ni sehemu ya mafanikio ya NWF katika kipindi hicho,” alisema Mtendaji huyo.

Aliyataja mafanikio mengine ya Mfuko wa Taifa wa Maji kuwa ni pamoja na ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita 200,000 lililopo katika Kata ya Tindingoma, wilayani Momba mkoani Songwe, ujenzi wa bwawa la New Sola lilipo katika Vijiji vya Zanzui, Mwabayanda na Mwashegheshi, Maswa, mkoani Simiyu.

Aidha, katika taarifa hiyo, Mtendaji Mkuu huyo alisema kwa sasa chanzo kikuu cha fedha kwa Mfuko Maji ni tozo ya mafuta ya Shilingi 50 kwa kila lita ya petroli na dizeli, tozo ambayo inatozwa kwa Mujibu wa Sheria ya Fedha Namba 16 ya Mwaka 2015.

“Katika kujenga uwezo wa taasisi zinazotekeleza miradi ya maji, Maofisa 150 kutoka Ofisi za RUWASA, Mamlaka za Maji na Bodi za Maji za Mabonde ya Mikoa ya Rukwa, Songwe, Iringa, Njombe, Mbeya, Sumbawanga, Shinyanga, Kigoma, Ruvuma na Morogoro, wamepatiwa mafunzo ya kuandaa maandiko ya miradi ya maji,” alisema.

Kuhusu Majukumu ya Mfuko wa Taifa wa Maji, Haji Mohammed aliyataja kuwa ni pamoja na kutafuta rasilimali fedha za utekelezaji wa miradi ya usambazaji majisafi na ulinzi wa vyanzo vya maji, pamoja na kutuma kwa watekelezaji wa miradi fedha kwa ajili ya miradi ya usambazi majisafi na ulinzi wa vyanzo vya maji nchini.

Majukumu mengine ni kufuatilia ya matumizi ya fedha kwenda kwa watekelezaji wa miradi kwa ajili ya miradi ya maji, kujenga uwezo wa kutekeleza miradi kwa taasisi zinazotekeleza miradi nchini na kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *