DAR ES SALAAM, TANZANIA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob John Mkunda, makamanda, wapiganaji wastaafu, wanafamilia na Watanzania kutokana na kifo cha Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali David Bugozi Musuguri.
Jenerali Musuguri amefariki dunia jijini Mwanza leo Jumanne Oktoba 29, alikokuwa akitibiwa, ambapo amefariki akiwa na umri wa miaka 104, kwani alizaliwa Januari 4, 1920 huko Butiama mkoani Mara, na alilitumikia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuanzia Mwaka 1942 hadi 1988.

Kutokana na msiba huo mzito, Rais Dk. Samia ametuma salamu za pole, akisema: “Kwaheri, Jenerali. Ninatoa salamu za pole kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob John Mkunda, Makamanda, wapiganaji wastaafu, wapiganaji walio katika utumishi, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote.
“Kwa kuondokewa na shujaa wetu, mpendwa wetu, mwalimu, mshauri na kiongozi wetu, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstaafu, Jenerali (Mstaafu) David Bugozi Musuguri.
“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha yake ya miaka 104, ambapo miaka 46 kati ya hiyo ameitumikia nchi yetu kwa weledi, umahiri, kujituma, ushujaa, nidhamu na kwa mafanikio ya hali ya juu, akiishi kiapo chake cha kuwa tayari kuutoa uhai wake ajili ya ulinzi wa Taifa letu.

“Ametuachia mfano bora wa utumishi wa umma utakaoendelea kuwa mwanga ndani na nje ya Majeshi yetu. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, Amiina” imemaliza taarifa ya Rais Samia aliyochapisha katika WhatsApp Channel yake saa 7:00 mchana wa leo.
Wakati wa uhai wake, Jenerali Musuguri lianza kazi yake kijeshi katika Jeshi la King’s African Rifles (KR) na Tanganyika Rifles, kabla ya kujiunga na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Jenerali Musuguri atakumbukwa zaidi kwa kuongoza majeshi ya Tanzania katika vita dhidi ya Idi Amin Dada wa Uganda Mwaka 1978, baada ya uvamizi wa eneo la Kyaka, mkoani Kagera na kulitangaza kuwa ni miliki ya Uganda.
Aliongoza Makamanda wenzake na wapiganaji chini ya Amiri Jeshi Mkuu wa wakati huo, Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kushusha kichapo kilichomfanya Idi Amini aiache ardhi ya Tanzania eneo la Kyaka na kurudi Uganda.

Kwa kuwa alizoea vitisho kwa Tanzania kwa kudai Kagera ni eneo la Uganda, Majeshi ya Tanzania chini ya Jenerali Musuguri yaliamua kumchapa Amini hadi nchini mwake Uganda na katika mji wake mkuu Kampala na kumfukuza kabisa katika ardhi ya Uganda na kwenda kuishi Uhamishoni nchini Saudi Arabia.
Ukiondoa vita vya Kagera, mapambano na vita aliyoshiriki ni pamoja na Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Battle of Madagascar na Battle of Simba Hills.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa, Jina lake lihimidiwe.