NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), imezindua Duka la Kisasa la Viatu liitwalo Renzo Shoe Plaza, huku ikimpongeza mmiliki na kuwataka wafanyabiashara wengine nchini kutumia fursa za usaidizi wa mamlaka hiyo ili kukua kiuchumi na kibiashara.

Renzo Shoe Plaza liko makutano ya mitaa ya Tandamti na Sikukuu, Kariakoo jijini Dar es Salaam, eneo ambalo ni kitovu cha biashara nchini, ambalo limezinduliwa na Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Bi. Latifa Khamis, ambaye alisema ushiriki wao unalenga kusapoti juhudi za Watanzania.

Akimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Suleiman Jafo, Bi. Latifa aliipongeza Renzo Shoe Plaza kufungua duka hilo kubwa, bora na la kisasa na kwamba anaamini linaenda kuwa suluhu ya changamoto ya Watanzania wanaohitaji viatu bora na vya kisasa kiasi cha kuagiza nje ya nchi.
“Sisi kama Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania, tunatoa fursa za kushirikiana na wafanyabiashara mbalimbali, jukumu letu ni kusimamia biashara za Watanzania kuhakikisha tunapromoti bidhaa zao na kusapoti jitihada zao,” alisema Bi. Latifa na kuongeza:
“TanTrade tuko hapa kwa jukumu moja kubwa, sisi ni wasimamizi wa biashara na tuna jukumu la kuhamasisha biashara miongoni mwa Watanzania, ni wajibu wetu kumtangaza Renzo, kuwajulisha Watanzania kwamba sisi tuko tayari kusaidia wafanyabiashara waweze kutumia fursa hizo.”

Bi. Latifa aliongeza ya kwamba moja kati ya majukumu ya taasisi yake ni kuhahakisha wanapromoti wafanyabiashara wa Kitanzania na biashara zao kwa ujumla na kwamba wanamkaribisha Renzo Shoe Plaza kushiriki Maonesho ya Sabasaba yanayoandaliwa na TanTrade.
“Sisi ndio waandaaji wa Maonesho ya Sabasaba, hivyo tunatumia fursa hii kuwakaribisha wafanyabiashara kama Renzo na wenzao, kuja kutumia ‘platform’ zetu mbalimbali, tunawapongeza sana kwa kuja na wazo hili, ambalo ni mwarobaini wa uhaba wa bidhaa bora na imara za viatu kwa Watanzania,” alisema.
Mkurugenzi huyo alitoa wito kwa Watanzania kuendeleza ubunifu wa kibiashara ili kukidhi mahitaji ya soko na wateja kwa ujumla na kwamba wao wapo tayari kushirikiana nao katika kuhakikisha wanafikia malengo yao kibiashara na kutoa mchango katika pato la taifa.





