Na Selemani Msuya
MAKAMU wa Rais Dk. Philip Mpango ameiomba sekta binafsi kuwekeza kwenye uzalishaji wa nishati jadidifu ya jotoardhi ambayo ni safi na salama kwa mazingira, huku akizitaka nchi za Afrika kuunganisha nguvu katika eneo hilo ili kuachana na matumizi ya nishati chafu.
Dk. Mpango ametoa wito huo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika (ARGeo) linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo la siku saba lina kauli mbiu isemayo “Kuharakisha Maendeleo ya Rasilimali za Jotoardhi Afrika” linashirikisha jumla ya washiriki 800 kutoka mataifa 21 duniani.
Makamu wa Rais amesema Tanzania ina rasilimali ya nishati ya jotoardhi ya kutosha katika mikoa zaidi ya nane, hivyo kuwataka wawekezaji kuja kuwekeza kwa kuwa watafaidika.
Kupitia kongamano hilo Makamu wa Rais ametaja baadhi ya maeneo ambayo utafiti umeonesha yana nishati ya jotoardhi ni pamoja na Ngozi (Megawati 70), Kyejo – Mbaka (Megawati 60), Songwe (Megawati 5-35), Natron (Megawati 60) na Luhoi (Megawati 5).

“Tanzania ipo tayari kwa ajili ya uwekezaji katika sekta ya jotoardhi kutokana na kuwa na amani na utulivu, mazingira mazuri ya kuvutia, utulivu wa kisiasa pamoja na sera imara chini ya marekebisho ya kimuundo kupitia falsafa ya 4R za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambazo ni maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya,” alisema.
Pia Dk Mpango ameitaka ya Wizara ya Nishati, Shirika la Kuendeleza Jotoardhi (TGDC) na wadau wengine kukaa pamoja na taasisi za kifedha na ndani na nje ili kuhakikisha fedha za utekelezaji wa miradi ya kuzalisha jotoardhi zinapatikana ambapo mikakatimya serikali hadi 2030 ni kuwa na megawati 5,000 za jotoardhi.
Makamu wa Rais alitumia nafasi hiyo kuishauri Taasisi ya Jotoardhi Afrika (AGA), kuandaa program ambazo zitawezesha rasilimali hiyo inazalishwa katika maeneo ambayo ipo kwenye Bara la Afrika.

Kwa upande mwingine Dk Mipango ametoa rai kwa nchi zenye rasilimali ya jotoardhi kushirikiana ili kuhakikisha zinapeana ujuzi wa namna ya kupata nishati hiyo ambayo ni endelevu.
Amesema nchi ya Kenya imefanikiwa kwa kiwango kikubwa ambao kwa sasa imezalisha zaidi ya megawati 1,000 za jotoardhi, hivyo ni vema kusaidia nchi zingine ambazo zimeanza mchakato wa uzalishaji.
“Nchi ambazo zimefanikiwa katika eneo hilo zinapaswa kubadilishanaji maarifa, mbinu bora, teknolojia, kubuni na kutekeleza programu za uchunguzi za kikanda. Wenzetu Kenya wamepiga hatua sana tuwatumie kuchochea utafutaji na uzalishaji wa jotoardhi,” alisema.
Makamu wa Rais amesema ni vema kwa kila nchi mwanachama kuwa na taasisi inayosimamia na kuongoza maendeleo ya jotoardhi ikiwa ni pamoja na mifumo sahihi ya kisheria na udhibiti ambayo inaweza kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi.
Makamu wa Rais amesema Tanzania imekamilisha hatua za awali za utafiti wa rasilimali ya jotoardhi katika maeneo matano yaliyo kando ya bonde la ufa, na imeanza kuchimba visima upande wa Magharibi mwa Ziwa Ngozi .
Amesema mafanikio mengine ni kuongezeka kwa idadi ya Watanzania wenye utaalam wa jotoardhi na ununuzi wa mitambo ya kuchimba visima.
Aidha, amesema kila nchi inapaswa kuwa na Taasisi maalum kwa ajili ya kusimamia uendelezaji wa Nishati ya Jotoardhi na kuwa na kanuni na sheria madhubuti zitakazowezesha sekta binafsi kushiriki katika uendelezaji wa nishati hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Kazi Maalum, Kapteni George Mkuchika amesema chini ya Rais, Samia sekta ya nishati imezidi kupiga hatua ambapo umeme vijijini umefika kwa takriban asilimia 98 na ifikapo Desemba mwishoni vijiji vyote vitakuwa vina umeme..
Ameeleza kuwa hali hiyo ni kielelezo cha mahitaji ya umeme kuongezeka hivyo lazima uendelezaji wa vyanzo mchanganyiko vya nishati uongezeke ikiwemo Jotoardhi ambayo ikiendelezwa itaweza kuzalisha umeme wa megawati 5000.
Awali, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga alimshukuru Rais, Samia kwa kujitoa kwake katika kuendeleza sekta ya nishati ambapo kwa sasa ni kiongozi wa kampeni ya nishati safi ya kupikia Afrika.

Amesema nishati ya Jotoardhi ni suluhisho muhimu katika utatuaji wa changamoto za upatikanaji wa nishati ya kutosha barani Afrika ambayo inaenda sambamba na mipango ya dunia katika kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa.
Waziri wa Maji, Nishati na Madini kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Shaibu Kaduara amesema kongamano hilo ARGeo ni muhimu kwa kuwa linaenda kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia na utunzaji wa mazingira.
Kaduara amesema Zanzibar inatumia zaidi ya megawati 150 za umeme kutoka Tanzania Bara ila kwa sasa kuna upungufu wa megawati 70, hivyo megawati 5,000 za jotoardhi zitakuwa mkombozi kwao.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Mafuta kutoka Kenya, James Wandayi amesema asilimia 46 ya nishati ya umeme Kenya inayotokana na jotoardhi, hivyo kuzitaka nchi zenye fursa hiyo kujikita katika kuzalisha.
Wandayi amesema Kenya ina zaidi ya megawati 1,000 ya nishati ya jotoardhi, hali ambayo inapunguza gharama ya umeme.

“Nishati ya jotoardhi ni nafuu, ila kubwa kuliko inachochea ukuaji wa uchumi na huduma za kijamii, tuwekezeni huko, sisi Kenya tupo tayari kutoa mafunzo kwa nchi ambayo unataka,” amesema.
Kwa upande wao wawakilishi wa mashirika ya kimataifa kutoka Umoja wa Mataifa (UN) Ofisi ya Tanzania, Mark Schreiner, Mwakilishi wa UNEP Afrika na Rais wa AGA, Dk Peter Omenda wamesema watashirikiana na nchi zote zinataka kuzalisha jotoardhi kwa kuwa ni nishati safi na salama katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.