NA MWANDISHI WETU
TUME ya Madini Tanzania imetoa ripoti ya mafanikio katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassani, ambayo inaonesha kukua kwa Ukusanyaji wa Maduhuli kutoka Sh. Bilioni 624.6 mwaka 2021/22 hadi Sh. Bilioni 753.8 mwaka 2023/24.
Ripoti hiyo imetolewa na kuwasilishwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhan Lwamo, alipokutana na Wahariri wa Vyombo vya Habari jijini Dar es Salaam Oktoba 24, ikiwa ni mfululizo wa mikutano ya Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, kueleza mafanikio yao.

Mhandisi Lwamo alisema Sekta ya Madini ni miongoni mwa nyenzo muhimu katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo ya kijamii na Taifa kwa ujumla na kwamba mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita ni kielelezo cha uongozi imara na madhubuti wa Rais Samia.
Akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari, Mhandisi Lwamo alisema ukuaji katika sekta hiyo utasaidia kuongeza Mapato ya Serikali na kukua kwa Mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa kufikia asilimia 10 ifikapo 2025.
Mhandisi Lwamo alifafanua kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Dk. Samia, alisema lengo la makusanyo ya tume yake kwa mwaka 2024/25 ni Sh. Trilioni 1, ambayo ni sawa na wastani wa kukusanya Sh. Bilioni 83.33 kwa mwezi katika mwaka huo wa fecha.
“Katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba, 2024, jumla ya kiasi cha Sh. Bilioni 257.89 kimekusanywa, na makusanyo hayo ni sawa na asilimia 103.16 ya lengo kwa kipindi husika, na pia ni sawa na asilimia 25.79 ya lengo la Mwaka 2024/2025,” alisema Mhandisi Lwamo katika taarifa yake.
Katika suala zima la Ushirikishwaji wa Wananchi, Mhandisi Lwamo alisema jumla ya Mipango 1,036 ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini iliidhinishwa kati ya mipango 1,050 na kwamba jumla ya ajira 19,356 zilizalishwa na kampuni 18,853 za Watanzania na 503 za Wageni.

“Bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.78 ziliuzwa migodini, ambapo Kampuni za Watanzania ziliuza bidhaa zenye thamani ya Dola Bilioni 3.46 (sawa na asilimia 91.68) na za Wageni Dola Bilioni 0.31 (sawa na asilimia 8.32),” alibainisha Mhandisi Lwamo.
Kwa upande wa Uwezeshaji kwa wachimbaji wadogo, Mhandisi Lwamo alisema Ttume yake imeweza kutoa elimu ya ugani kuhusu usalama, afya, mazingira, pamoja na usimamizi wa baruti ili kuwa na uchimbaji salama na endelevu, ambako jumla ya Wachimbaji 867,124 walinufaika.
Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema katika Utoaji na Usimamizi wa Leseni za Madini, kulikuwa na Mwenendo Chanya wa utaoji leseni tangu mwaka 2021/2022 hadi 2024/2025, ambako tume yake ilitoa leseni kubwa 4 kwa Kampuni za Mamba Minerals, Tembo Nickel Refining, Sotta Mining na Graphite Corp. Ltd.
Katika Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Tume ya Madini iliyo chini ya Wizara ya Madini iliyoanzishwa Mwaka 2017 chini ya Sheria ya Madini Sura 123, ilifanya kaguzi katika migodi mikubwa tisa kati ya kaguzi 144 na migodi midogo 47,535, pamoja na Usimamizi wa stoo na maghala ya baruti.
Taarifa ya Mhandisi Lwamo iliyataja Maeneo ya vipaumbele kwa tume yake kuwa ni pamoja na kuimarisha mazingira ya utendaji kazi wa Tume ya Madini, kuimarisha usimamizi wa Sekta ya Madini na ukusanyaji wa Mapato ya Serikali yatokanayo na rasilimali madini.
“Pia, maeneo ya vipaumbele ni pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa ukaguzi wa usalama, afya, mazingira na uzalishaji wa madini katika migodi midogo, ya kati na mikubwa, pamoja na kuendelea kuboresha mazingira ya kuwawezesha wananchi kunufaika na rasilimali madini,” alifafanua Mhandisi Lwamo.
