BENKI ya NMB na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wamesaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano, unaolenga Kukuza Vipaji, Ubunifu, Uwekezaji katika Mageuzi ya Kidigitali na Msaada wa Kifedha kwa wanafunzi wa Chuo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Co-ICT), kilicho chini ya chuo hicho.

Makubaliano hayo ya miaka mitano, yamesainiwa leo Jumatano Oktoba 23 Makao Makuu ya NMB jijini Dar es Salaam, UDSM ikiwakilishwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Utafiti Profesa Nelson Boniface na NMB imewakilishwa Afisa Mkuu wa Rasirimali Watu, Emmanuel Akonaay

Akizungumza kabla ya kusaini mkataba huo, Akonaay alisema NMB ambayo elimu ni sekta ya kipaumbele, inaamini kuwa makubaliano hayo yanaenda kuchochea ubunifu miongoni mwa wanafunzi wa Co-ICT, ambao utawezesha utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoizunguka jamii na taifa kwa ujumla.
Alibainisha ya kwamba makubaliano hayo yatajikita katika maeneo matano ya; Ukuzaji Vipaji na Ujuzi, Ukuzaji Ubunifu wa Matumizi ya Teknolojia, Uwekezaji katika Mageuzi ya Kidigitali, Utafiti Teknolojia na Maarifa, pamoja na Msaada wa Kifedha wa Masomo kusaidia programu bunifu.
“Katika Ukuzaji wa Vipaji na Ujuzi, kwa pamoja NMB na Co-ICT tutashirikiana katika kutambua na kuendeleza kupitia mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika Nyanja za TEHAMA, kama itakavyokuwa kwenye Ukuzaji wa Ubunifu wa Matumizi ya Teknolojia.

“Hapo tutasaidia kuendeleza ushindani katika Sekta ya Fedha ambayo inakua kwa kasi sana, pande zote zitashirikiana katika kutoa fursa kwa wanafunzi kujaribu teknolojia tofauti zinazoweza kuwa na athari chanya kwa sekta ya kifedha kupitia SANDBOX,” alifafanua Akonaay.
Aliongeza ya kwamba, katika Mageuzi ya Kidigitali, NMB na Co-ICT kwa pamoja watawekeza kwenye nyanja hiyo ili kuongeza ufanisi, kupunguza gharama na kuboresha huduma kwa wateja na katika Utafiti wa Teknolojia na Maarifa, watashirikiana kufanya utafiti wa kiteknolojia ili kuchunguza athari zake kwa Sekta ya Fedha.
