DAR ES SALAAM, TANZANIA
MAMIA ya wasanii wakongwe na chipukizi wa Sanaa za maigizo (Bongo Movie na Vichekesho – Comedy), wamejitokeza kwa wingi kushiriki shughuli mbalimbali na maziko ya msanii nguli Yusuf Abdallah Kaimu ‘Mzee Pembe.’

Dua na swala ya maiti vimefanyika nyumbani kwa marehemu Yombo Dovya CCM na baadaye mazishi kufanyika katika Makaburi ya Msikiti Mweupe uliopo mkabala na Shule ya Msingi Yombo Dovya wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.

Mkongwe Abdallah Mkumbila ‘Muhogo Mchungu,’ aliongoza mamia ya wasanii hao, ambapo kamera za Habari Mseto ziliwanasa nyota hao wakiwemo Lucas Mhavile ‘Joti,’ Lumole Matovolwa ‘Biggie,’ na Ulimboka Mwalulesa ‘Mzee Senga,’
Wasanii wengine walioonwa na kamera ya Habari Mseto katika maziko hayo ni pamoja na Khamis Changalwe ‘Mtanga,’ Seif Mbembe ‘Mzee Mbembe, Rashid Mwinshehe ‘Kingwendu,’ Vicent Kigosi ‘Ray,’ Hemed Khalfan Maliyaga Mkwere na Fatuma Makongoro ‘Bi Mwenda.’
Mkali wa Bongo Fleva, Haruna Kahena ‘Inspekta Haroun na Lidai Madebe ni miongoni mwa wasanii nyota waliohudhuria Dua, swala ya maiti na maziko ya Mzee Pembe, aliyeacha mke na watoto 10. Mungu amlaze pema marehemu Mzee Pembe, Hakika Sisi ni wa Mwenyezi Mungu na Kwake Tutarejea.

