DAR ES SALAAM, TANZANIA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amewazawadia Sh. Mil. 20 yoso wa timu ya soka ya taifa ya vijana chini ya miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes,’ baada ya kutwaa ubingwa wa Michuano ya Kufuzu Mataifa ya Afrika kwa Vijana (AFCON U-20), Kanda ya Afrika Mashariki.

Ngorongoro Heroes wanaonolewa na Charles Boniface Mkwasa, wametawazwa mabingwa wa michuano hiyo baada ya kuichapa Kenya kwa mabao 2-1, kwenye dimba la KMC, jijini Dar es Salaam, uwanja ambao waliutumia kuwavua taji Uganda katika nusu fainali.
Dakika 45 za kwanza ziliisha kwa sare tasa, kabla ya Kenya kupata bao la uongozi dakika ya 48, lakini nyota wawili vijana wanaochezea klabu kongwe za Simba na Yanga, Valentino Mashaka na Shekhan Ibrahim, kuibeba Ngorongoro Heroes kwa kuifungia mabao mawili (daakika za 63 na 79) yaliyowapa taji hilo.

Ushindi huo sio tu umeiwezesha Ngorongoro Heroes kulipa kisasi cha kufungwa bao 2-1 katika ufunguzi dhidi ya Kenya hao hao, bali pia wamefanikiwa kutwaa taji linalowapeleka AFCON U-20 wakiwa mabingwa kwa huu unaosimamiwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Mwenyeji wa fainali hizo za mwakani zinazotambulika kama 2025 TotalEnergies U-20 Africa Cup of National, atajulikana kesho Oktoba 22 katika upigaji kura utakaoenda sambamba na Mkutano Mkuu wa CAF, utakaofanyika jijini Addis Ababa nchini Ethiopia. Bingwa wa Afrika wa AFCON U-20, atafuzu Kombe la Dunia.
Aidha, yoso Sabri Kondo wa Ngorongoro Heroes, anayechezea timu ya KPZ ya Zanzibar, ametwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano hayo, ambayo huenda fainali zake zikafanyika nchini Morocco, taifa ambalo litakuwa mwenyeji wa fainali za AFCON 2025 kwa wakubwa.
