Msajili wa Hazina achangisha Mil. 117/- za Ujenzi wa Kanisa la KKKT K’njaro

Kilimanjaro, Tanzania

MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu, ameendesha Harambee ya kukusanya fedha za kuendeleza ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Naibili, Siha, mkoani Kilimanjaro, ambako aliwezesha kuchangisha kiasi cha Sh. Mil. 117.8, zikiwemo pesa taslimu na ahadi.

Mchechu ambaye ni kiongozi mwenye mchango mkubwa katika uongozi, hususani Sekta za Nyumba, Benki na biashara, ameendesha Harambee hiyo kwa ajili ya jengo la ibada ambalo ujenzi wake ulianza miaka sita iliyopita.

Katika harambe hiyo iliyofanyika Jumapili ya leo Oktoba 20, Mchechu alichangisha pesa taslimu kiasi cha Sh. Mil. 50.2, huku kukiwa na ahadi za Sh. Mil. 66.5, wakati Sh. Mil. 1.1 zilipatikana kwa njia ya mnada. Pia, harambee hiyo iliwezesha upatikanaji mifuko 118 ya saruji.

Pesa hizo na saruji ni kwaajili ya upauaji wa jengo hilo la ibada na kazi ya plasta, ambapo kwa mujibu wa Askofu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Fredrick Shoo, kazi hizo mbili zinatarajiwa kugharimu kiasi cha Sh. Mil. 150.

Akizungumza na viongozi wa kidini, serikali na kijamii, pamoja na waumini wa Naibili, Mchechu alisisitiza kuwa ipo haja ya kuendelea kuwa na moyo wa kutoa na kushirikiana mpaka ujenzi wa nyumba hiyo ya ibada utakapokamilika.

“Tunapoendelea na ujenzi huu, nataka niwaombe ninyi wapendwa msiishie hapa. Tuendelee kufanya kazi kwa pamoja mpaka ujenzi utakapokamilika.

“Kanisa bado linahitaji michango yenu, maombi yenu, na utayari wenu wa kujitoa. Kila mmoja wetu anaweza kutoa kitu, iwe ni fedha, muda, au huduma kwa namna yoyote ile,” alibainisha Mchechu

Aliongeza ya kwamba, ikiwa watatoa kwa moyo wa upendo, Mungu atarudisha zaidi na zaidi na vikombe vyao vitafurika.

Akinukuu vifungu vya Biblia Takatifu, Mchechu alisisitiza kwa kunukuu Luka 6:38, mstari usemao: “Wapeni watu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa, cha kusukwasukwa, na kushindiliwa, na kufurika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu.”

Aliongeza: “Kama vile Nehemia alivyowaongoza watu wa Yerusalemu kujenga tena ukuta wa mji baada ya kuharibiwa, ninyi pia muendelee kujitoa kwa uaminifu na bidii katika ujenzi wa nyumba ya Mungu.”

Kwa upande wake, Dk. Shoo, alisema matamanio yao ni kuona wanakamilisha plasta, kuweka madirisha, milango na madhabahu, kupaka rangi na kuanza maandalizi ya kutengeneza samani, ifikapo mwaka 2026.

Aliongeza kuwa hadi kufikia hatua hii ya kabla ya upauaji, kiasi cha Sh. Mil. 229.8 kimeshatumika, shukrani kwa watu wenye mapenzi mema na Mungu kwa michango yao.

Askofu Shoo alisema baada ya upauzi na plasta, awamu ya pili ni kujenga madhabahu, madirisha na milango ya mbao.

“Baada ya hapo awamu inayofuata itakuwa kuweka tarazo, bodi ya dari, kusuka umeme na rangi, huku awamu ya nne ikiwa ni kuweka viti na kumalizia madhabahu kwa kutumia mbao.

“Awamu ya mwisho itakuwa ni kufunga vifaa vya muziki, mifumo ya kamera za ulinzi na usalama ‘CCTV Camera’, kiyoyozi na mfumo wa TEHAMA,” alifafanua Dk. Shoo na kuongeza:

“Ni wakati mwafaka wa kushirikiana kufanya kazi hii ya baraka iliyopo mbele yetu. Mungu atutie nguvu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *