TASNIA ya Sanaa ya uchekeshaji nchini, imepata pigo baada ya mchekeshaji mkongwe Tanzania, Yusuph Kaimu maarufu kwa jina la Pembe, kufariki dunia leo Oktoba 20, 2024.

Taarifa ya kifo chake imethibitishwa na wasanii mbalimbali akiwemo Vicent Kigosi ‘Ray,’ na mchekeshaji Tin White, ambao wametumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kutoa taarifa za kufariki kwa Pembe.
Taarifa za awali zinadokeza kuwa, Pembe ambaye alikuwa akiishi Yombo Dovya wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, amefariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Temeke, alikokuwa akitibiwa.
Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Mkoa wa Dar, Francisco Mwinuka ‘Pierre,’ amethibitisha na kueleza anaelekea Hospitali ya Temeke, huku akiahidi kwamba taarifa zaidi zitatolewa baadaye.
