Wakati Taifa Stars ikisuasua, Ngorongoro Heroes yafuzu AFCON 2025

DAR ES SALAAM, TANZANIA

WAKATI timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars,’ ikijiweka njiapanda kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), kikosi cha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes,’ kimefuzu fainali za michuano hiyo kwa vijana, baada ya kuwazabua yoso wa Uganda kwa mabao 2-1 jijini Dar es Salaam jioni hii.

Ngorongoro Heroes inayonolewa na kocha Charles Boniface Mkwasa ‘Master,’ imeibuka na ushindi katika nusu fainali ya kusaka tiketi ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), iliyopigwa kwenye dimba la KMC, Mwenge Dar es Salaam, ambako wenyeji hao walitoka nyuma kwa bao 1-0 na hatimaye kushinda kwa mabao 2-1.

Shujaa wa Ngorongoro Heroes aliyeibeba Tanzania mabegani kuipeleka AFCON ya vijana 2025 alikuwa ni Jamny Simba, aliyefunga bao la ushindi dakika ya 119, baada ya Sabri Kondo kuisawazishia bao kunako dakika ya 70, hivyo kulazimisha pambano kwenda katika dakika 120.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *