DAR ES SALAAM, TANZANIA
UMOJA wa Wanawake wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Boko jijini Dar es Salaam, umetembelea na kukabidhi msaada wa vifaa tiba na mavazi vyote vikiwa na thamani ya Sh. Mil. 10 kwa Wodi ya Watoto wanaotibiwa saratani kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika katika Wodi ya Watoto Wenye Saratani MNH, ikihudhuriwa na Mchungaji wa KKKT Usharika wa Boko, Ambakisye Lusekelo, ambaye alisema kutoa ni agizo la Yesu Kristo linalopaswa kutekelezwa na kila mmoja kwa nafasi yake.

Akizungumza wakati hafla hiyo fupi, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa KKKT Usharika wa Boko, Mary Lemma, alianza kwa kumshukuru Mungu kwa nafasi ya kuwa miongoni mwa wachache katika jamii ambao wameelekeza mikono yao kutoa kwa wenye uhitaji.
“Tumekuwa tukisaidia wenye uhitaji katika Wodi ya Saratani hapa Muhimbili tangu mwaka 2018, ambapo tumekuwa tukifika kuwasaidia mahitajhi ya msingi hasa yale wanayotuambia tuwaletee, na leo tumekuja hapa kukabidhi vifaatiba mbalimbali na mavazi vyenye thamani ya Sh. Milioni 10.
“Tumeleta ‘bedside lockers’ 10 yanayokaa pembeni mwa vitanda vya wagonjwa, tumeleta ‘BP Monitor’ mbili za Watoto, ‘Multi Table,’ moja, ‘Infusion Pump,’ moja na majora ya nguo za watoto wa kike na wa kiume wanaotibiwa hapa.
“Haya ni sehemu ya mahitaji tuliyoambiwa tulete, tunaushukuru uongozi wa Hospitali ya Muhimbili kushirikiana nasi katika kufanikisha hili, wito wetu ni kwa jamii ya Watanzania, kujitokeza kusaidia watoto hawa, ambao wana uhitaji mkubwa sana,” alisema Mary Lemma.
Awali, Mchungaji wa KKKT Usharika Boko, Ambakisye Lusekelo, alisema Umoja wa Wanawake wa kanisa lake wamekuwa na utaratibu wa muda mrefu wa kufanya ziara hapo kusaidia mahitaji ya msingi ya Watoto hao na kwamba kwa kufanya hivyo wanatekeleza agizo la Yesu Kristo.

“Tumekuwa tukiwatembelea, tumekuwa na urafiki nao, sio wao tu, bali hata na madaktari wao, manesi na wazazi wao. Hili ni agizo la Yesu Kristo mwenyewe aliyesema ‘Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie kwa maana Ufalme wa Mbingu ni wao.
“Lakini pia, tunakumbushwa kuwa Dini iliyo safi ni kuwatembelea watu wenye uhitaji na Yesu Kristo anasema; ‘Kadri ulivyowatendea walio wadogo, ulinitendea mimi.’ Kwa hiyo tumekuja kutimiza agizo la Yesu mwenyewe,” alifafanua Mchungaji huyo.