Bashe azindua kituo atamizi Mkonge BBT, aagiza Bodi kuweka vifaa vya kisasa

Waziri wa Kilimo Huseein Bashe (katikati) akiongozana na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge, Saady Kambona kukagua ujenzi wa kituo hicho.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (kulia) akizindua rasmi ujenzi wa kituo hicho atamizi cha Mkonge.

Na Mwandishi Wetu, Tanga

WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe
ameiagiza Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), kuweka utaratibu mzuri kuhakikisha
kunakuwa na vifaa vyote muhimu katika Kituo Atamizi cha Mkonge BBT kilichopo Tanga.

Waziri Bashe amesema hayo jana baada ya kuzindua Kituo hicho
kinacholenga kutoa mafunzo ya ubunifu na uzalishaji wa bidhaa za mkono zitokanazo na
singa za Mkonge, uzalishaji nzi chuma,
utengenezaji wa karatasi, mafunzo ya ukataji na uchakataji Mkonge.

Amesema kituo hicho kinahitaji kuwa na vifaa ili wanawake wenye ulemavu na vijana wanaozalisha bidhaa mbalimbali wakija wakute vifaa vyote muhimu ambapo pia
watatumia kituo hicho kama sehemu ya kuzalishia mali na kufanya biashara zao nje.

“Naagiza tupate vifaa vyote muhimu
ambavyo vinahitajika kwa ajili ya kufanya shughuli ndogo ndogo za uzalishaji mkonge ili vikundi vya wajasiriamali kina mama na vijana
wakipata mkopo wa asilimia 10 wa
halmashauri, wana uwezo wa kwenda
kununua singa za Mkonge au malighafi
hawahitaji kununua mashine, watazikuta
hapa.

“Mkonge ni zao muhimu sana katika uchumi wa nchi, zipo bidhaa nyingi zinazotokana na
mkonge. Bodi imeingia makubaliano na wenzetu ambao wamekuwa wakifundisha namna ya kutumia mabaki ya Mkonge katika
kuzalisha karatasi,” amesema Bashe.

Amesema serikali imeweka
dhamira kupitia maombi ya bodi takribani Sh milioni 600 kwa ajili ya kuweka Kituo Atamizi Tanga na Zanzibar ambapo Tanga itakuwa
kituo ambacho vitawekwa vifaa vyote vidogo vidogo vya kuongeza thamani ya Mkonge na
mazao mengine ya kilimo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mkonge wa TSB, Olivo Mtung’e amesema Kituo hicho kimeanzishwa Tanga kwa sababu Mkonge unalimwa zaidi na ndiyo Makao Makuu ya TSB.

Amesema lengo la kituo hicho ni kuwawezesha vijana, wanawake na
wenye ulemavu kwa ajili ya kujiajiri lakini pia watakwenda kuwasaidia ambao wanazalisha
Mkonge hasa kwa upande wa Tanga ambao walikuwa wanakosa soko la kuuza Mkonge nje.

“Soko letu bado linategemea zaidi kuuza nje huku ndani matumizi siyo makubwa sana
lakini tunatambua kuwa vijana wetu, kina mama hawana ajira za kuwaingizia kipato kwa hiyo tunategemea kituo hiki kuwa na watu
ambao watajiajiri. Pia tutaongeza matumizi ya zao la Mkonge kwa upande wa ndani.

“Lakini pia kituo hiki ni sehemu ya kwanza tu kuna vituo vingi vinakuja kutakuwa na mashine ya kutengeneza bidhaa za mkono za kufuma kama vile Kamba na cha pili kinaratajiwa kuanzishwa hapa hapa Tanga kwa ajili ya kutengeneza karatasi na gypsum
na vitu vya kuezekea,” amesema Olivo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *