Kilimanjaro, Tanzania – Leo, Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) limedhihirisha tena ahadi yake ya kuimarisha usalama wa chakula kwa kutangaza mradi wa Feed the Future Tanzania Tuhifadhi Chakula. Mradi huu wa miaka mitano, wenye thamani ya Shilingi za Kitanzania bilioni 60 (Dola za Kimarekani Milioni 24), unalenga kupunguza upotevu wa chakula baada ya mavuno katika minyororo ya thamani ya kilimo cha mboga mboga na nafaka nchini Tanzania. Mradi unatekelezwa na Chama cha Kilimo cha Mboga Mboga Tanzania (TAHA) na Kituo cha SAGCOT. Wakati wa uzinduzi, USAID kwa kushirikiana na wakulima, wafanyabiashara, na wasindikaji walionesha juhudi zao za pamoja za kupambana na hasara na upotevu wa chakula. Hafla hii ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa David Silinde, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, na Balozi wa Marekani Michael Battle.
“Tunasherehekea ushirikiano ambao utaongeza usalama wa chakula, kuboresha hali za maisha, kuunda ajira, na kutoa fursa za kuuza nje ya nchi, hasa kwa wanawake na vijana,” alisema Balozi Battle. “Kupitia miradi kama hii na Mpango mpya wa kupunguza Upotevu wa Chakula, Tanzania inatarajia kupunguza hasara za baada ya mavuno kwa asilimia 50 katika maeneo yanayolengwa na programu. Ushirikiano huu unatarajiwa kuleta hadi dola milioni 20 za uwekezaji kwa ajili ya viwanda vya usindikaji na matumizi bunifu ya mabaki ya kilimo.”
Tangu ulipoanzishwaa mwezi Agosti 2023, mradi wa Feed the Future Tanzania Tuhifadhi Chakula umekuwa na manufaa makubwa, ikiwa ni pamoja na kuimarisha soko la ndizi la Kilimanjaro, ambapo tani 216,000 ziliwafikia wanunuzi, kupunguza hasara baada ya mavuno, na kuzalisha karibu Shilingi milioni 400 za Kitanzania kama mapato kwa wakulima wa eneo hilo.
Mradi huu utajumuisha zaidi ya wahusika 930,000 katika minyororo ya thamani – wakiwemo wakulima, wasindikaji, wafanyabiashara, na taasisi za kifedha – kote Tanzania. Utatekelezwa kuanzia Agosti 2023 hadi Julai 2028, na utaendeshwa katika mikoa kumi ya Tanzania (Morogoro, Njombe, Pwani, Tanga, na Zanzibar, Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, na Kilimanjaro).
Uzinduzi wa mradi wa Feed the Future Tanzania Tuhifadhi Chakula unafuatia tangazo la Septemba 19 lililotolewa na Msaidizi wa Rais wa Marekani kwa Masuala ya Usalama wa Taifa Jake Sullivan na Msimamizi Mkuu wa USAID na Mratibu wa Feed the Future Samantha Power, kwamba serikali ya Marekani, ikishirikiana na Bunge la Marekani, imejitolea zaidi ya dola milioni 80 za fedha mpya za Feed the Future na rasilimali za ziada, ikiwemo dola milioni 13 za msaada wa ziada kwa Tanzania. Fedha hizi zinaunga mkono Mpango wa Kuboresha Upatikanaji Chakula, juhudi ya kuimarisha ushirikiano wa Marekani katika usalama wa chakula na kuzingatia rasilimali katika nchi tatu za Afrika ya Kusini na Mashariki.
Chini ya Mpango wa Kukuza Chakula, uwekezaji wa Marekani utatumia ardhi yenye rutuba, mifumo mbalimbali ya kilimo, na ari ya serikali kutaka mabadiliko, ili kusaidia eneo la kilimo kuwa ukanda wa uzalishaji chakula. Hali hii itaweza kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi katika nchi husika, huku ikiimarisha ustahimilivu wa wazalishaji na mifumo dhidi ya mabadiliko na matatizo ya kieneo. Utafiti wa hivi karibuni umeonyesha kuwa kuongeza mavuno ya nafaka kwa asilimia 25 katika Afrika Mashariki na Kusini kunaweza kuongeza thamani ya uzalishaji wa kilimo katika eneo hilo kwa zaidi ya dola bilioni 24 kufikia mwaka 2030 na kupunguza njaa kwa watu milioni 22.