Serikali yaipongeza NMB kudhamini Kariakoo Festival 2024

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, (wanne kushoto) akipokea zawadi ya kuchorwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kutoka kwa Msanii wa uchoraji, Adolf Shirima, ikiwa ni zawadi maalum kwa Mhe. Rais iliyokabidhiwa wakati wa ufungaji wa Tamasha la Kariakoo Festival, lililomalizika leo Sept 21/ 2024 kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini dar es Salaam. Tamasha hilo lililofanyika kwa muda wa siku saba lilidhaminiwa na Benki ya NMB na kushirikisha wafanyabiashara mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na Taasisi za Serikali. Kutoka 9Kushoto) ni Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Seka Urio, Mkuu wa Idara ya Biashara Benki ya NMB, Alex Mgeni na Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Kariakoo, Martin Mbwana. (Na Mpiga Picha Maalum).

Mkuu wa Idara ya Biashara Benki ya NMB, Alex Mgeni, akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara walioshiriki katika Tamasha la Kariakoo Festival (hawapo pichani) wakati wa kufunga Tamasha hilo lililofungwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, lililomalizika leo Sept 21/2024 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Da res Salaam. Tamasha hilo lililofanyika kwa muda wa siku saba lilidhaminiwa na Benki ya NMB na kushirikisha wafanyabiashara mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na Taasisi za Serikali.

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imeipongeza Benki ya NMB kwa kudhamini Tamasha la Wafanyabiashara wa Kariakoo ‘Kariakoo Festival 2024,’ huku ikizitaka taasisi za fedha nchini kuiga mfano wa benki hiyo katika uwezeshaji wafanyabiashara wadogo, wa kati na wajasiriamali kuchangia Uchumi na Pato la Taifa.

Pongezi hizo na wito vimetolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe wakati wa ufungaji wa Kariakoo Festival Jumamosi, tamasha lililowakutanisha pamoja wadau wa biashara Kariakoo, ili kuuza na kununua bidhaa kwa bei punguzo, na kuwaunganisha na wateja wa ndani na nje ya nchi.

Akizungumza wakati wa kufunga tamasha hilo, Naibu Waziri Kigahe alisema NMB inaastahili pongezi na inapaswa kuigwa kwa kufanikisha uwepo wa jukwaa hilo la uwezeshaji kukua kiuchumi kwa wafanyabiashara wa Kariakoo

Naibu Waziri Kigahe alisema Kariakoo ni eneo kimkakati, akilitaja kuwa ni kitovu cha biashara nchini, kinachoiingiza TRA mapato ya zaidi ya Sh. Bil. 2 kwa siku, hivyo mchango wowote wa kuwainua zaidi wafanyabiashara wa eneo hilo, unapaswa kutambuliwa, kuthaminiwa na kuheshimiwa na Serikali.

“Moja ya changamoto kubwa tulizonazo kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wetu, ni mitaji, kufanikisha tamasha hili ni kuwafungulia fursa sio tu za kujuana, bali kushirikiana na kupeana mbinu mpya za kibishara na upatikanaji wa mikopo nafuu ili kukua kiuchumi na kuongeza mchango wa malipo yao ya kodi.

“Wito wangu kwa taasisi zingine za fedha ni kuiga mwenendo huu wa NMB, kusaidia maendeleo ya biashara, sisi kama wizara furaha yetu ni kuona wajasiriamali na wafanyabiashara wanafanikiwa, na nyinyi wafanyabiashara na wajasiriamali, mnapaswa kuwa waadilifu na waaminifu kwa NMB.

“Kopeni, fanyieni kazi na hakikisheni mnalipa mikopo ili kuwapa imani na uwezo wa kukopesha wengine, msitumie hili neno Teleza Kidijitali, kuteleza na mikopo ya NMB, mtakwamisha wakopaji wengine,” alisema Naibu Waziri Kigahe.

Alisisitiza kuwa taasisi zingine za fedha nchini zinapaswa kuiga hili, kwani wafanyabiashara nchini sio tu wana akaunti NMB pekee, kwani kila benki ina kada hiyo muhimu, lakini linapokuja suala la uwezeshwaji, wanaoonekana kuitikia ni NMB tu.

Mkuu wa Idara ya Biashara ya NMB, Alex Mgeni, alisema benki yake imewakopesha wafanyabiashara zaidi ya Sh. Trilioni 2.5 katika kipindi cha miaka miwili, kipindi ambacho wametoa pia mikopo ya Mshiko Fasta kwa wateja wa benki hiyo inayofikia Sh. Bilioni 120.

“Wakati tukiombwa kudhamini, tulikumbushwa kuwa hili ni eneo la kimkakati kibiashara, nasi kama NMB tuna matawi mengi na wateja, hii ikatusukuma kuona ipo haja ya kufanikisha kutaniko lao.

“Tuna matawi matano Kariakoo kati ya matawi 231 Tanzania nzima na mpango uliopo ni kuongeza idadi hiyo hapa.

“Takwimu zinaonesha, NMB tuna wafanyabiashara wenye akaunti zaidi ya 400,000 na katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, tumetoa mikopo yenye thamani ya Sh. Trilioni 2.5 kwa kada hiyo muhimu kwa maendeleo ya uchumi,” alisema Mgeni.

Alibainisha ya kwamba NMB imefanya uwekezaji mkubwa katika ubunifu na teknolojia, huku akiitaja moja ya bunifu hizo kuwa ni Teleza Kidijitali, mwamvuli wa huduma za kifedha kwa njia ya mtandao, ambao Naibu Waziri wa Viwanda na Uwekezaji, Exaud Kigahe alikiri kuvutiwa nao.

“Teleza Kidijitali ilikuwa ni kampeni tuliyoendesha kwa miaka miwili, ikilenga kuwahamisha wateja matawini, wapatie huduma kidijitali na moja ya bidhaa gumzo tunazotoa kidijitali ni Mshiko Fasta, mikopo nafuu isiyo na dhamana wala ujazaji fomu, unaokuwezesha kukopa hadi Sh. Mil. 1.

“Mikopo hii inawasaidia sana kina baba na mama lishe wanaohitaji uwezeshaji fulani ashubuhi, wauze mchana na jioni warejeshe na kupitia Mshiko Fasta, hadi sasa NMB imeshakopesha kiasi cha Sh. Bilioni 120 kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wengineo kwa muda wa miaka miwili,” alisema.

Mgeni aliongeza ya kwamba, licha ya huduma hizo zote, Kariakoo Festival walikuwa na bidhaa inayofanya vizuri sokoni hivi sasa ya Lipa Namba, ambayo haina gharama kwa mfanyabiashara, wala haina makato yoyote kwake, kwani gharama na makato hubaki kwa mnunuzi tu.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo (JWK), Martin Mbwana, aliishukuru NMB kwa kulipokea wazo lao la uanzishwaji wa Kariakoo Festival, kisha kukubali kuwa mdhamini mkuu, na kwamba wanatambua na kuthamini mchango wa taasisi hiyo katika kuwainua kiuchumi.

NMB ilikuwa Mdhamini Mkuu wa tamasha hilo, lililojumuisha sio tu wafanyabiashara wa Kariakoo, bali taasisi za umma zinazofungamana na biashara zikiongozwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), zikiwemo Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).

Taasisi zingine ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), (Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), Shirika la Viwango Tanzanaia (TBS), Tume ya Ushindani (FCC) na Shirika la Bima la Taifa (NIC).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *