Washindi Watatu wa Shindano la Teknolojia la Marekani na Tanzania Watangazwa

DAR ES SALAAM – 20 Septemba, 2024 – Asasi tatu ambazo ni Jamii Forums, Smart Foundry Ltd na The Launchpad Tanzania leo zimetangazwa washindi wa Shindano la Teknolojia la Marekani na Tanzania, shindano lililowakutanisha wanateknolojia vinara, asasi za kiraia, taasisi za kielimu na vyombo vya Habari ili kutatua changamoto na kutafuta suluhisho za kibunifu katika nyanja za ushiriki wa raia, kujenga ufahamu kuhusu dhima na utendaji wa vyombo vya habari (media literacy).

Kupitia shindano hili, Jamii Forums itapokea Dola za Kimarekani 100,000, Smart Foundry itapokea Dola za Kimarekani 80,000 na Launchpad Tanzania itapokea Dola za Kimarekani 70,000.

Mgeni Rasmi Jerry Silaa, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia, alitoa hotuba ya ufunguzi katika hafla iliyohudhuriwa pia na Mwakilishi wa UNESCO nchini, Michel Toto, Naibu Balozi wa Marekani Nchini Andrew Lentz, na Daniel Kimmage, Naibu Mratibu Mkuu wa Global Engagement Center.

“Ushirikiano kama tulionao hivi leo – kati ya maafisa wa serikali, wajasiriamali kutoka sekta binafsi, wavumbuzi na wabunifu wa teknolojia, na watumiaji wa teknolojia hizo – unaweza kuhamasisha ubunifu mkubwa unajao na juhudi za ushirikiano zitakazoweza kujenga mustakabali wetu wa pamoja,” alisema Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dk. Michael A. Battle. “Kwa pamoja tunaweza kuimarisha miundombinu ya kimataifa ya habari iliyo huru na wazi.”

Likizinduliwa mwezi Juni, shindano hili la teknolojia la Marekani na Tanzania linatafuta suluhisho za kibunifu kutoka kwa mashirika ya Kitanzania ili kukuza uadilifu na kuaminika kwa taarifa, kuongeza ushiriki na kujihusisha zaidi kwa raia katika shughuli za kiraia, na kuimarisha ujuzi na maarifa yanayohitajika kutafuta na kutafsiri habari katika enzi ya kidigitali.

Zaidi ya maingizo 100 yalipokelewa na kutathminiwa, na washiriki nane waliingia fainali. Hapo Septemba 18, washiriki hawa nane waliwasilisha jinsi teknolojia zao zinaweza kutatua changamoto muhimu katika sekta ya habari mbele ya jopo la majaji kutoka Marekani na Tanzania. Septemba 19, washindani walioingia fainali, waliungana na zaidi ya washiriki 200 wakiwemo wanaharakati wa asasi za kiraia, viongozi wa biashara, wataalamu wa teknolojia, na maafisa wa serikali katika mfululizo wa mijadala na mawasilisho ya mada mbalimbali kuhusu changamoto za kiteknolojia. Pia walijadili mustakabali wa teknolojia nchini Tanzania, matumizi ya akili bandia, na jinsi ya kujipatia mapato kutokana na biashara zao za teknolojia na namna ya kuifikia mitaji ya kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *