DAR ES SALAAM, TANZANIA
WAZIRI wa Afya, Jenister Mhagama, amefanya ziara ya kwanza ya kikazi katika taasisi bobezi na bingwa za matibabu, ikiwemo Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), ambako amekiri kuvutiwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Jenister Mhagama aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Afya Agosti 15 mwaka huu kuchukua nafasi ya Ummy Mwalimu, amesema ziara yake hiyo ililenga kuoanisha huduma za taasisi hizo zinavyowafikia wananchi na mapokeo yao, ambako alijionea ufanisi unaotokana na mapinduzi ya kisekta yaliyoletwa na Serikali.
Akizungumza na wanahabari alipokuwa MOI, Waziri Mhagama alisema kupitia ziara hiyo, amejifunza ama kujionea uwekezaji mkubwa sana uliofanywa na Serikali ya Rais Dk. Samia, kwenye taasisis hizo, ambako fedha nyingi sana imewekezwa kwenye vifaatiba, mashine na hata miundombinu.

“Hii ni ziara yangu kubwa ya kwanza tangu nilipoteuliwa na nimeamua kuanza na taasisi hizi kubwa tano zinazotoa tiba za kibingwa na kibobezi. Kikubwa hapa nilichokuwa nataka ni kuonisha huduma zinazotolewa na taasisi hizi na namna zinavyoweza kuwafikia wananchi na mapokeo yake kwa jamii.
“Nimeshuhudia Pamoja nanyi, uwekezaji mkubwa sana, kuna mashine nyingi, bora na za kisasa zinazotumia teknolojia ya hali ya juu, kwa mfano hapa MOI, kuna mashine zinazowapa uwezo wa kutibu mishipa, uwezo wa kufumua kichwa na kutibu uvimbe wa aina yoyote kichwani.
“Miaka mitatu iliyopita, huduma hizo zilikuwa haziwezi kufanyika nchini, zilikuwa ni tiba zilizokuwa zikipatikana nje ya nchi tu,” alisema Waziri Mhagama.
Aliongeza ya kwamba ajali za barabarani, zikiwemo za bodaboda zimeongezeka sana, ambako kupitia ziara hiyo, amejionea namna wagonjwa kwenye wodi walivyoathiriwa sana mifupa yao na ajali hizo, lakini zimeshafanyika tiba sahihi za kibobezi kwa majeruhi hao.
Waziri huyo alijivunia uwekezaji huo unaoifanya taasisi kama MOI kuwa ni tegemezi na maarufu sana katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, kutokana na huduma zake.
“Vile vile, pale JKCI, uwekezaji mkubwa mno umefanyika pale, huku kukiwa na mashine zinazowezesha kufanya Upasuaji wa kutumia matundu na mgonjwa akapata nafuu, akatibiwa magonjwa ya moyo na mishipa ambayo damu imeziba na kadhalika,” alibainisha Waziri Mhagama.