Wakala wa Vipimo yateta na Wahariri Tanzania kueleza mafanikio, changamoto

Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa WMA, Alban Kihulla, akizungumza katika mkutano wa Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kuelezea utendaji kazi wa wakala huo.

Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Ilala, Muhono Nashon (kulia) akifafanua jambo kwa Wahariri namna wanavyoweza kugundua Mita za Maji zilizochezewa na watu wasio wahaminifu.

Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa WMA, Alban Kihulla, akionesha kipimo kisicho rasmi cha nyanya ambacho kimekuwa kikitumiwa na wafanyabiashara wengi.

DAR ES SALAAM, TANZANIA

WAKALA wa Vipimo Tanzania (WMA), umekutana na Wajumbe wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kuwaeleza mafanikio iliyopata katika kipindi cha mwaka mmoja, huku ikiahinisha changamoto zinazoikabili, ikiwemo idadi ndogo ya waajiriwa wa kudumu.

WMA iliyoanzishwa Mei 17, 2002 ikiwa chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, imekutana na Wahariri hao Jumatano Septemba 11, ilikowaeleza juu ya Historia ya Wakala, Ofisi ilizonazo, Majukumu, Mafanikio, Changamoto na Mpango Mkakati wa mbeleni.

Akizungumza katika mkutano huo, ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kuelezea mafanikio ya taasisi za Serikali, Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa WMA, Alban Kihulla, alisema miongoni mwa mafanikio yao ni kuongeza kwa mchango wake katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Kihulla alibainisha ya kwamba, Wakala imeongeza mchango huo kwa kiwango cha 4.3 mwaka 2022/23 kutoka 4.2 cha Mwaka wa Fedha wa 2021/22, pamoja na kuongezeka kwa Idadi ya Vipimo Vinavyohakikiwa na Kuendelea na Ununuzi wa Vifaa vya Kitaalam.

“Katika kila mafanikio hapakosi changamoto, iko hivyo pia WMA, ambayo miongoni mwa changamoto tulizonazo ni kungeza Uelewa Kuhusiana na Matakwa ya Sheria ya Vipimo, Maboresho ya Mazingira ya Ufanyaji Biashara nchini, Pamoja na Mabadiliko ya Teknolojia.

“Lakini pia, WMA inakabiliwa na uwepo wa watumishi wachache wa ajira kudumu, ambapo waliopo ni 267, wakati mahitaji ni kuwa na watumishi 581, ikiwa na maana kuna upungufu wa watumishi 314,” alisema Kihulla mbele ya wahariri hao.

Kwa upande wa Mpango Mkakati wa WMA kwa siku za usoni, Kihulla alisema ni pamoja kuingia kwenye maeneo mapya ya uhakiki wa vipimo, kutoa elimu kuhusiana na Matakwa ya Sheria ya Vipimo, kuboresha mifumo ya utendaji kazi, pamoja na kujenga uwezo (mafunzo na ununuzi wa vifaa).

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tazania (TEF), Deodatus Balile, aliipongeza kwa mafanikio iliyopata, lakini akaitaka kuitumia vema fursa ya ushirikiano wao na vyombo vya habari kuwafikia wananchi ili kuwawezesha kutumia bidhaa zinazokidhi mahitaji ya kisheria katika vipimo na ujazo.

“Niwaombe WMA, ingawa sijui bajeti yenu ikoje, lakini manaweza kutenga kiasi cha pesa kuhakikisha vyombo vya habari vinashiriki kampeni zenu mbalimbali, cha kuzingatia ni kuwa bajeti mtakayotenga itarudi mara nyingi kupitia elimu mtakayotoa na kufikisha kwa jamii.

“Bajeti hiyo ni uwekezaji, kama tunavyoona Kampuni za Simu zikijenga minara kwa gharama kubwa, lakini zinarudi kupitia mapato yatokanayo na usimikaji wa minara hiyo,” alisisitiza Balile na kuongeza kuwa WMA inayo kazi kubwa ya kufanya katika kuziba mianya ya udanganyifu katika vipimo.

“Kwa kweli kuna shida klubwa katika vifaa vya ujenzi, ambako nondo tunazoambiwa ni futi 40, kiuhalisia ni futi 35 na nusu, mabati tunayoambiwa ni mita tatu, ni mita mbili pointi saba au nane tu. Hapa mnayo kazi ya kufanya kuhakikisha usahihi wa vipimo unakidhi sheria,” alisema Balile.

Aliongeza kuwa wizi huo uliokithiri ni mkubwa katika bidhaa mbalimbali, ikiwemo misumari, dawa za kuchua, dawea za meno, dawa mbalimbali za vidonge na zile za maji na kwamba madhara ya hilo ni makubwa, kwani matumizi yake yanakuwa sio sahihi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *