Ongezeko la mizigo  bandarini  lamkuna Makala

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) imesema kuwa uwekezaji uliofanywa na DP World katika Bandari ya Dar es Salaam wenye thamani ya takriban dola milioni 250 ( sawa na bilioni 675) kwa ajili ya uendeshaji wa magati 0-7 umeonyesha mafanikio makubwa ndani ya kipindi cha miezi mitatu  ambapo  shehena ya makasha imeongezeka kutoka 7,151 mwezi Aprili 2024 hadi kufikia 20,151 kufikia mwezi Julai 2024.

Akiwasilisha ripoti fupi ya utendaji wa bandari hiyo baada ya uwekezaji huo kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Amos Makala, wakati wa ziara yake  badarini jana, Meeneja wa Shughuli  na Uratibu wa TPA,  Josephat Lukindo amesema pesa hizo imetumika kuboresha utendaji wa bandari hiyo katika maeneo matatu baada ya kukabidhiwa na mamlaka ya bandari Aprili 15, 2024.

“Kwa uzoefu tulionao wa katika uendeshaji wa bandari, tuliamua kuanza na uboreshaji wa maeneo matatu muhimu  ili kuongeza ufanisi zaidi,” amesema Lukindo.

Amesema sehemu ya kwanza kabla ya kufanya kitu chochote kampuni ya DP World kupitia kampuni tanzu ya DP World Dar es Salaam iliyoanzishwa kusimamia bandari hiyo  ilifanya manunuzi ya mitambo ya kisasa yenye thamani ya takriban bilioni 215.

Alisema pili ilifanya ukarabati wa mitambo mibovu iliyokuwa ikitumika bandarini hapo na kufanya manunuzi ya vifaa vipya yakiwemo matrekta ya kubebea mizigo 20 pamoja na matela 31, jenereta  saba zenye ukubwa wa Kv 10,000 kila moja kwa ajili ya kuendeshea mitambo ikitokea umeme umekatika na vifaa vya kubebea mizigo mizito (cranes) .

“Tatu, DP World ilifanya usimikaji wa mifumo ya kisasa ya TEHAMA kwa ajili ya utendeshaji wa bandari hiyo.“Hapo awali, tulikuta mifumo ambayo imepitwa na wakati na kuamua kuweka mifumo ya kisasa kuendana na maendeleo ya teknolojia,” amesema.

Hivyo, amesema uwekezaji huo umeleta manufaa makubwa ndani ya kipindi cha miezi mitatu iliyochangia  ongezeko la shehena ya makasha  ikiwa sawa  na   ongezeko la asilimia 18.2.

Akifafanua zaidi, meneja huyo, alisema idadi ya meli zinazosubiri baada ya kutia nanga zimepungua kutoka meli  mbili hadi sifu , meli  za kichele (zinazobeba bidhaa kama mbole na nafaka) nazo zimepungua kutoka meli saba  hadi meli moja na zile zinazobeba mzigo mchanganyiko pia zimepungua kutoka meli 17 hadi nane kwa kipindi cha miezi mitatu baada ya uwekezaji huo mkubwa.

“Uwekezaji huu utaifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa katika ushindani na bandari nyingine kubwa barani Afrika ikiwemo ya Morocco,” amesema na kuongeza kuwa TPA inatekeleza kwa vitendo  4R za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Akiongea baada ya ziara yake bandarini hapo, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Makalla alipongeza utendaji kazi wa TPA  na kufurahishwa na  mafanikio haya akielezea kuwa ni kielelezo tosha kwa wale waliokuwa wanaubeza uwekezaji huo.

“Kuna watu wao kazi yao ni kupinga  kila kitu.“ Hata wakati Serikali inanunua ndege walipinga pia na cha ajabu wanafurahia kupanda ndege hizo hivi sasa,” alisema Makala na kuongeza kuwa wengine walipinga uwekezaji wa treni ya SGR na hata  ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere kwa ajili ya kuzalisha umeme.

Amesema CCM inaiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita inayoongwa na Dkt Samia kwa uwekezaji huo katika maeneo yote muhimu ikiwemo bandari kwani hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya CCM.

“Tupo katika ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya uwekezaji  iliyotekelezwa na serikali ukiwemo wa Bandari ya Dar es Salaam na kiukweli tumekoshwa sana na maendeleo tuliyaona,” amesema.

Akiongea kwa niaba ya  Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, Naibu Mkurugenzi wa TPA, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Juma Kijavala amesema mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi kifupi cha uwekezaji wa DP yametokana na hatua mbalimbali zilizochukua ili kuongeza ufanisi wa utendaji na kuvutia wafanyabiashara zaidi wa ndani na nje ya nchi.

“Bandari ya Dar es Salaam itakuwa na uwezo wa kushindana na bandari nyingine duniani kwa kutoa huduma bora na kwa haraka kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika,” amesema Kijavala.

Miongoni mwa mikakati ya kuifanya bandari hiyo iwe shindani ni pamoja na ujenzi wa gati na matanki ya kuhifadhia mafuta na bidhaa zinazoharibika haraka (perishable)  kama vile mbogamboga ili zihifadhiwe na kupelekwa nje ya nchi.

Amesema TPA pia inaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa gati la kuhudumia watalii itakayokuwa na uwezo wa kuhudumia watalii milioni mbili kwa kuanzia.

Amesema kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa,  bandari hiyo inazidi kutanua soko lake la kimataifa ambapo nchi ya Sudan Kusini pia imeonesha nia ya kuitumia bandari hiyo.

“Tunajivunia ukubwa wa soko wa bandari yetu ambapo kwa ujumla inahudumia takriban watu milioni 700 katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki na Kati na ni mategemeo yetu kuwa idadi hii itaongezeka,”amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *