Majaliwa: Tanzania iko tayari kushirikiana na Cuba kujenga kiwanda kikubwa cha chanjo

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Rais wa Kiwanda na Kituo cha Utafiti cha Biocuba Farm cha nchini Cuba Bi. Mayda Mary’s baada ya kutembelea kiwanda na kituo hicho kinachotengeneza chanjo za magonjwa mablimbali, Agosti 13, 2024. Wa pili kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humfrey Polepole. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

0872 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitembelea kiwanda na kituo cha utafiti kinachotengeneza Viatilifu na Viuadudu cha Labiofam kilichopo Boyeros nchini Cuba, Agosti 13, 2024. Kulia kwake ni rais wa kiwanda na kituo hicho Rod Manuel Valdes. Waziri Mkuu alikuwa katika ziara maalum ya kuboresha mahusiano kati ya Tanzania na Cuba. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Kiwanda na Kituo cha Utafiti kinachotengeneza Viatilifua na Viuadudu cha Labiofam kilichopo Boyeros nchini Cuba alipokitembelea, Agosti 13, 2024. Wa tatu kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, wa pili kulia ni Rais wa kiwanda hicho Rodi Manuel Valdes na kushoto ni Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Yordenis Despaigne Vera. Mheshimiwa waziri Mkuu alikuwa katika ziara maalum yakuboresha mahusiano kati ya Tanzania na Cuba. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania  iko tayari kushirikiana na Serikali ya Cuba kujenga kiwanda kikubwa cha kuzalisha chanjo mbalimbali ikiwemo chanjo ya  homa ya ini.

Amesema viwanda vya dawa nchini Cuba vikiwemo vinavyotengeneza dawa zinazotokana na mimea tiba vimeiwezesha nchi hiyo kupunguza utegemezi wa  kuagiza dawa kutoka nje ya nchi hiyo  kwa asilimia 60 .

Ameyasema hayo Agosti 13, 2024 alipotembelea kiwanda na kituo cha  Utafiti cha LABIOFAM kilichopo nchini Cuba ambacho kinazalisha bidhaa mbalimbali za binadamu, kilimo na mifugo. Waziri Mkuu alikuwa  nchini Cuba  katika ziara maalumu  ya kuboresha mahusiano kati ya Tanzania na nchi hiyo.

Alisema kiwanda hicho kinashirikiana na kiwanda cha Viuadudu cha Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC)  cha LABIOFAM kilichopo Kibaha mkoani Pwani  ambacho kinatengeneza viuadudu  vitakavyopulizwa kwenye mazalia ya mbu nchini kote  na  Afrika ili kuangamiza mbu na kutokomeza ugonjwa wa maralia.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuielekeza Wizara ya Afya ishirikiane na Ubalozi wa Tanzania uliopo Havana nchini Cuba kuandaa ziara itakayowezesha kufanyika mazungumzo na Wizara ya Afya ya Cuba, viwanda, taasisi na mashirika yanayotengeneza dawa mbalimbali nchini humo.

Mheshimiwa Majaliwa alisema lengo la mazungumzo hayo ni kuweka utaratibu mzuri  utakaowezesha dawa hizo kuuzwa nchini baada ya  kupata vibali kutoka vyombo na taasisi zenye dhamana ya  kuidhinisha matumizi ya dawa nchini.

Mheshimiwa Majaliwa alizitaja dawa hizo kuwa ni pamoja na  dawa za kutibu maumivu ya viungo (Rheumatoid Arthititis)  na dawa ya kutibu vidonda kwenye miguu kwa watu wanaokuwa na ugonjwa wa kisukari.

Waziri Mkuu alisema kiwanda cha Labiofam kinazalisha  bidhaa mbalimbali za binadamu, kilimo na mifugo ambazo kutokana na ubora na umuhimu wake zinatumika katika nchi mbalimbali.

Awali, Waziri Mkuu alitembelea kiwanda kingine  kikubwa na Kituo cha Utafiti cha CIGB  kinachotengeneza bidhaa mbalimbali za afya na tiba.

Katika ziara hiyo Mheshimiwa Majaliwa aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Balozi Hamphrey Polepole.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *