FURAHA YA WATANZANIA NI KUPATA UMEME WA UHAKIKA – DKT. BITEKO

 TANESCO Tumieni umeme uliopo kufanya matengenezo


 Asema Rais Samia ameweka msukumo kuimarisha sekta ya Nishati


 TANESCO Kujenga vituo vya kanda kudhibiti mifumo ya umeme

Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza
mara baada ya kutembelea Kituo cha Kuzalisha Umeme wa Gesi Ubungo I, II
na III pamoja na Kituo cha Kudhibiti umeme wa Gridi ya Taifa leo Agosti
11, 2024 jijini Dar es Salaam.

 


Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

 


Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe Dkt. Doto Biteko ameliitaka
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kutumia fursa ya uwepo wa umeme wa
kutosha katika kipindi hiki  kufanya matengenezo ya mashine
mbalimbali ambazo hazikuweza kufanyiwa matengenezo kipindi ambacho nchi
ilikuwa haina umeme wa kutosha.

 

Dkt.
Biteko ameyasema hayo leo 11 Agosti, 2024 jijini Dar es Salaam wakati
alipofanya ziara ya kutembelea vituo vya umeme vya Ubungo I, Ubungo II,
Ubungo III pamoja na kituo cha kudhiti mifumo ya umeme wa gridi yaani
Grid control Centre.


Dkt. Biteko ameitaka TANESCO kuhakikisha  matengenezo ya miundombinu ya umeme yanakuwa endelevu ili watanzania wapate umeme wa uhakika.


‘’Kwakweli namshukuru Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa msukumo wake mkubwa katika  Sekta ya Nishati na sisi kama Wizara kupitia Tanesco tutaendelea kuhakikisha  watanzania wanapata umeme wa uhakika.’’ Amesema Dkt. Biteko


Amesema kwa sasa kuna ziada ya umeme na ndio maana  matengenezo yanaweza kufanyika  kwenye mitambo  katika
vituo vya Kidatu, Kihansi na Mtera na hivi karibuni TANESCO
itakamilisha matengenezo kwenye laini za Mikoa ya Kaskazini ili
kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme ambapo amewashukuru wananchi wa
mikoa hiyo kwa uvumilivu wao katika kipindi chote cha matengenezo.


Amesisitiza
kuwa, kwa sasa hali ya upatikanaji wa umeme ni ya kuridhisha hasa
ikizingatiwa kuwa mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere
unaendelea vizuri na tayari mashine tatu zimeshaungwa kwenye gridi ya
Taifa na mashine ya nne inatarajiwa kuingizwa mwezi huu na kwamba tayari
mashine tatu za mradi wa Rusumo zinafanya kazi.


Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Udhibiti Mifumo, Mha. Deogratius Mariwa
amesema kwa sasa TANESCO inafanya maboresho kwenye mfumo wake wa Gridi
ili uende sambamba na mahitaji ya sasa kwa kujenga vituo 5 vya kanda vya
kudhibiti mifumo ya gridi sambamba na vituo vya ziada vitakavyosaidia
wakati wa hitilafu za umeme.


Amesema
mipango iliyopo kwa sasa ni kuongeza vituo takribani 20 katika kipindi
cha miaka 3 sambamba na kuunganisha mifumo ya gridi na nchi za Kenya,
Uganda, Zambia na baadaye Msumbiji ili kuinarisha mifumo ya upatikanaji
umeme.


Amesema
Vituo hivyo vitajengwa kwenye mikoa ya Arusha, Mwanza, Dar es Salaam,
Mbeya na Dodoma ambapo kwa sasa wako kwenye hatua za kumpata mkandarasi
na kuongeza kuwa kwa sasa kuna jumla ya vituo 67 vya gridi.


Ziara
hiyo imehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi
Mramba, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio pamoja
na Menejimenti ya TANESCO.



Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *